ABUJA,NIGERIA

MAGENGE ya wabeba silaha wameua wanajeshi wasiopungua 23 nchini Nigeria katika kijiji kimoja kaskazini mashariki mwa nchi hiyo.

Taarifa zinasema kuwa hujuma hiyo ya kuvizia ilitokea Jumapili usiku wakati wanajeshi hao walipokuwa wakipita katika eneo la msitu la Wilaya ya Jibia jimboni Katsina.

Miili 23 ya wanajeshi hao ilipatikana huku baadhi ya wanajeshi wakiwa hawajulikani waliko.

Magenge ya wabeba silaha ambayo yalikuwa yakijihusisha na wizi wa mifugo na utekaji nyara yaliongezeka kaskazini mwa Nigeria na wataalamu wanaonya kuwa magenge hayo sasa yanashirikiana na kundi la kigaidi la Boko Haram.

Pia katika eneo hilo hilo, watoto watano waliuawa na wengine sita kujeruhiwa wakati bomu lililoporipuka.

Jimbo la Katsina, anakotoka Rais Muhammadu Buhari wa Nigeria, linakabiliwa na tatizo kubwa la umasikini na limekuwa likishuhudia mashambulizi ya mara kwa mara ya wahalifu na magaidi katika miaka ya hivi karibuni.

Kwingineko, Jeshi la Nigeria limetangaza kuwaangamiza magaidi nane wa ngazi za juu wa kundi la Boko Haram.

Msemaji wa Wizara ya Ulinzi ya Nigeria John Enenchi alisema magaidi hao waliuawa katika hujuma iliyotekelezwa kwa ndege za kivita katika kijiji cha Goski jimboni Borno.

Ni zaidi ya muongo mmoja sasa ambapo, eneo la kaskazini mashariki mwa Nigeria limekuwa uwanja wa mashambulizi ya wanachama wa kundi la kigaidi Boko Haram.

Zaidi ya watu elfu 30 wameuawa na wengine wanaokaribia milioni tatu walilazimishwa kuwa wakimbizi kutokana na mashambulizi ya kundi hilo la Boko Haram nchini Nigeria tokea mwaka 2009.