OUAGADOUGOU, BURKINA FASO

TAARIFA zinaeleza kuwa karibu wanajeshi wawili wameuwawa na wengine watano kujeruhiwa katika shambulizi lililotokea  huko Burkina Faso karibu na mpaka wa Niger.

Duru moja ililiambia shirika la habari la AFP kuwa shambulizi hilo limefanyika asubuhi mapema katika eneo la Tankoualou katika mkoa wa Komandjari huku taarifa nyengine zikieleza kuwa wanajeshi watatu walijeruhiwa vibaya.

Wiki iliyopita raia walishambuliwa katika mashambulizi mawili yaliyofanywa katika eneo hilo hilo.

Burkina Faso ilijikuta katika hali ya kukabiliwa na mashambulizi ya kigaidi yaliyoanzia katika nchi jirani  ya Mali na sasa kuna wasiwasi kuhusiana na usalama wa majimbo yaliyo kusini mwa nchi hiyo.

Burkina Faso ni mojawapo ya nchi maskini zaidi duniani na mashambulizi hayo ya kigaidi yalisababisha vifo vya zaidi ya watu elfu moja na karibu watu milioni moja kutoroka makaazi yao.