NA AHMED MAHMOUD, ARUSHA
WANANCHI zaidi ya elfu tatu kutoka kijiji cha Kikuletwa kata ya Mbuguni wilayani Simanjiro wanatarajiwa kunufaika na mradi wa kisima cha maji unaoanzia mkoani Manyara kwenda Arusha.
Wakizungumzia kuhusiana na mradi huo wananchi hao Janeth Apaeli na Ida Nanyaro, walisema kuwa mradi huo umekuja muda muafaka ambao wananchi hao walikuwa wakikumbana na changamoto ya kutembea umbali mrefu kufuata huduma ya maji.
Walisema kuwa, kukosekana kwa maji katika eneo hilo limekuwa ni changamoto ya Muda mrefu, kwani wanawake ndio wamekuwa wakipata shida kutokana na kuamka usiku kufuata maji, jambo ambalo linahatarisha maisha yao kutokana na usalama kuwa mdogo.
“Kwa kweli tunashukuru sana serikali kwa kuleta mradi huu katika eneo hili, mradi ambao umekuwa ni kilio cha muda mrefu kutokana na adha tunayoipata,” alisema.
Naye mkazi wa kijiji hicho, Barnaba Nabamo alisema kuwa, wamekuwa wakinywa maji ya visima ambayo sio salama kwa afya zao, ila uwepo wa maji hayo utasaidia sana kuwaondoa katika adha hiyo waliyokuwa wakikumbana nayo kwa muda mrefu.
Aidha watekelezaji wa mradi huo ni kampuni ya Shanxi Construction Engineering and Minerals Corporation ambao unasimamiwa na Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira jiji la Arusha kwa ufadhili wa Benki ya Maendeleo Afrika (AfDB).
Meneja mradi wa kampuni ya Shanxi construction Engineering and Minerals Corporation Li Zhi Xin alisema wanaishukuru serikali kwa kuwapa fursa ya kutekeleza mradi huo ambao unatarajiwa kukamilika mwakani.
Xin alisema kuwa changamoto wanayokabiliana nayo katika utekelezaji wa mradi huo ni mabadiliko ya tabia nchi hasa kipindi cha mvua ambapo husababisha mradi kuchelewa lakini wanajitahidi kuumaliza kwa wakati.
Nae Afisa Mwajiri wa kampuni hiyo, Janeth Saganya alisema kuwa mradi huo ulianza mwaka jana na unatarajiwa kukamilika Septemba mwaka huu huku ukiwanufaisha vijana mbalimbali kutokana na kutoa ajira katika utekelezaji wa mradi huo.