NA WAANDISHI WETU
WANACHAMA wa Chama cha Mapinduzi, wamekipongeza chama hicho kwa kumteuwa Dk. Hussein Mwinyi kuwa mgombea wa urais wa Zanzibar.
Wamesema wanaamini uteuzi wa mgombea huyo utaleta mafanikio makubwa kwa wazanzibari kutokana na kutumikia vizuri vipindi vitatu vya awamu tofauti akiwa serikalini.
Wakizungumza na Zanzibar Leo katika maeneo tofauti ya Zanzibar wanachama hao walisema, wana imani na CCM kwa kuchagua kiongozi mwenye sifa atakaesimamia vyema kwa maslahi ya chama na Taifa kwa ujumla wakati atakapochaguliwa.
Seif Amir Seif mkaazi wa Amani, ambae ni Mwenyekiti wa wazazi wilaya hiyo alisema, Dk. Hussein alitumikia nafasi hizo kwa ujasiri na kuonyesha upendo wa nchi yake kwa kufanya mengi mazuri, kuanzia awamu ya tatu ya Benjamin Mkapa, awamu ya nne ya Jakaya Kikwete na awamu ya tano ya Dk. John Magufuli.
“Kutokana na umahiri wa kazi zake, tuna imani kubwa wazanzibari tutapata kiongozi bora atakaeendeleza mazuri yaliyoachwa na rais wa awamu ya saba Dk. Ali Mohamed Shein ikiwemo kufuata nyayo zake”, alisema.
Alifahamisha kuwa, Chama cha Mapinduzi kimepata maendeleo ya kisiasa na kidemokrasia ambayo ni mfano mzuri kwa vyama vyengine na nchi nyengine duniani.
Naye, Ali Khamis Jabir mkaazi wa Kilimahewa, ambae aliwaomba wananchi wa Zanzibar wapenda amani na maendeleo kuunga mkono jitihada za CCM katika kumuunga mkono mgombea huyo wakati utakapofika kwa kumchagua kwa kura nyingi ili aweze kuitekeleza ilani atakayopewa na chama kwa maslahi ya wananchi.
Mtumwa Hassan Ali, mkaazi wa Fuoni, alisema uchaguzi wa kuteua mgombea wa nafasi ya urais ulienda vizuri kwani ulikua huru, uwazi na haki, hivyo hakuna budi kumkubali kuwa kiongozi wao atakaeongoza Zanzibar.
Aidha aliwataka wanawake waendelee kuhamasisha familia zao majumbani kuhusu kujitokeza kwa wingi kumpigia kura Dk. Hussein pale wakati utapofika.