NA ABOUD MAHMOUD

WANANCHI wa visiwa vya Zanzibar wamewapongeza vijana katika kujitokeza katika kuwania nafasi mbali mbali za uongozi ikiwemo Urais, Ubunge, Uwakilishi na Udiwani.

Wakizungumza na Zanzibar Leo wananchi hao walisema ni jambo jema lilioneshwa na vijana wa nchi hii katika kujitumbukiza kuwania nafasi hizo na kuonesha kutaka kuleta maendeleo.

Walisema kwamba kujitokeza kwao huko na kuchukua fomu kumedhihirisha kwamba vijana wameamka na kuona ipo haja ya kujitokeza kwa ajili ya kusaidia wenzao wakiwemo wazee.

“Mimi napongeza sana hatua iliyochukuliwa na vijana walianza kujitokeza tangu katika nafasi ya Urais hii ilinifurahisha sana nikaona sasa kweli vijana wameamka  na kuonesha nia njema katika nchi yetu,”alisema Haji Hussein.

Wananchi hao walisema kwamba ushirikishwaji wa vijana katika Serikali ya awamu ya saba ya uongozi wa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohammed Shein, na kuleta maendeleo kumeonesha kuwasukuma vijana wengi kujikita katika kuwania nafasi hizo za uongozi.

Amina Daud Simba ,mkaazi wa Fuoni alisema kwamba kujitokeza kwa vijana katika uchukuaji wa fomu za kuwania nafasi mbali mbali kumeonesha ishara njema kwa kuleta mabadiliko makubwa ya kimaendeleo.

“Nimefarijika sana kuona vijana wenzangu tena wanawake na wanaume wamekuwa wakijitokeza wakichukua fomu za kuwania nafasi mbali mbali naamini lengo lao ni kuleta maendeleo makubwa katika nchi yetu wakipata nafasi ya kuchaguliwa,”alisema Amina.