NA ABOUD MAHMOUD

WANANCHI wa visiwa vya Unguja wameipongeza Halmashauri Kuu ya Chama cha Mapinduzi (CCM) kwa kumchagua Dk. Hussein Mwinyi kuwa mgombea wa Urais wa Zanzibar katika uchaguzi Mkuu ujao, kupitia chama hicho.

Wakizungumza na Zanzibar Leo, kwa nyakati tofauti, wananchi hao walisema Halmashauri Kuu inastahili pongezi kwa kuchagua kijana na ataejua matatizo ya wananchi na kuyatatua na kuyaendeleza mazuri yatakayoachwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohammed Shein .

Wananchi hao walifahamisha kuwa imani ya wanachama wa Chama cha Mapinduzi na Wazanzibari  ipo kwa mgombea huyo Dk. Hussein Mwinyi  kutokana na mengi aliyoyafanya katika jimbo na chama chake.

“Imani yetu sisi Wazanzibari hivi sasa ipo kwa Dk. Hussein kwa sababu ndio chaguo la Halmashauri Kuu na sisi tunaamini kwamba atakua kiongozi imara, mchapakazi na asiependa majungu,”alisema Kassim Issa.

Dauhat Saleh, alifahamisha kwamba anaamini waliochukua fomu  kuwania nafasi hiyo wote walikuwa wazuri katika kushika madaraka, lakini imewalazimu kuchagua mtu mmoja ambae atakua mzuri zaidi.