NA MWAJUMA JUMA

WANARIADHA nchini wametakiwa kujiamini kwa kile wanachokifanya ili kuweza kufikia malengo ambayo wamejiwekea.

Wito huo ulitolewa na mchezaji wa zamani wa mchezo huo Masoud Tawakali alipokuwa akizungumza na mwandishi wa habari hizi huko Amaan.

Alisema  mchezaji mzuri ni yule ambae anajiamini na kuwa na malengo ya kufikia hatua fulani.

Alisema kama kweli wataweza kufanya hivyo kwa hakika itakuwa njia rahisi ya wao  kufanikiwa kama ambavyo wao waliweza.

“Mchezaji mzuri ni yule anaejijua nini anafanya, chezeni kwa malengo”, alisisitiza.

Tawakali alisema wakati wao wanacheza kila mmoja alikuwa na malengo yake aliyojiwekea jambo ambalo limewasaidia  kufanikiwa ingawa sio kwa asilimia kubwa.

“Hatukufikia kwa asilimia mia lakini kuna mambo nimeyapata ambayo kusema kweli yatakuwa ni historia kwangu na kwa wajukuu zangu”, alisema.

Alisema akiwa mchezaji alicheza kwa bidii ili kukamilisha malengo yake ikiwemo kupata ajira ambapo aliajiriwa na JWTZ na sasa mafanikio yake anayaona.

Hivyo aliwataka wachezaji hao kujituma na kuwa na ari ya kushiriki michezo mbali mbali, ili iwe chachu ya wao kupata ajira na kuendesha familia zao hapo baadae.