KAMPALA,UGANDA

WANASAYANSI wa Uganda  wameonya kwamba idadi ya watu wenye COVID-19 nchini inaweza kuongezeka kama watu hawatoendelea kuchukua hatua za kujilinda na virusi.

Wiki hii na wiki iliyopita Uganda ilirikodi vifo vya kwanza vya COVID-19 kwa  watu wawili, hivyo wanasayansi walionya kuwa maambukizi zaidi na vifo huenda vikatokea kama watu hawakufuata masharti ya umbali wa kijamii,kuvaa barakoa na kuosha mikono.

Waziri wa afya, Ruth Aceng alisema mtu mmoja anayethibitishwa, kama hakuhudumiwa mapema,anaweza kueneza virusi haraka, na kuathiri maelfu ya watu.

Alionya kuwa kama idadi itakuwa kubwa sana vituo vya afya na watumishi wa afya wataelemewa, na kupelekea vifo vingi zaidi.

Hadi Julai 29, Uganda ilirikodi jumla ya watu wenye COVID-19 1,147, ambapo 1,028 wameshapona na vifo viwili.