KINSHASA,CONGO

WATU wanne wameuawa na wengine kadhaa wamejeruhiwa katika maandamano ya kupinga uteuzi wa mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Tume ya Pamoja ya Kutetea Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa (UNJHRO),ilithibitisha mauaji hayo na kulaani kitendo cha polisi ya DRC cha kutumia nguvu kupita kiasi kuzima maandamano ya wananchi.

Katika maandamano hayo, askari polisi walitumia mabomu ya gesi ya kutoa machozi kuzima maandamano hayo ya ghasia baina ya wafuasi wa Rais Felix Tshisekedi wa nchi hiyo na makundi ya kiraia yanayopinga uteuzi wa mwenyekiti mpya wa Tume Huru ya Kitaifa ya Uchaguzi (CENI).

Aidha  Tume ya Pamoja ya Kutetea Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa ililaani mauaji ya askari polisi mmoja katika maandamano hayo ya ghasia yaliyoshuhudiwa katika mji mkuu Kinshasa, Lubumbashi, Goma na miji mengine midogo ya nchi hiyo.

Kambi ya upinzani na makundi ya kiraia ya nchini humo yanapinga uteuzi wa Ronsard Malonda kuwa Rais wa CENI, kuwa ni mpambe wa aliyekuwa rais wa nchi hiyo Joseph Kabila.

Uteuzi wa Malonda ulipasishwa wiki iliyopita na Bunge la nchi hiyo ambalo wanachama wake ni wafuasi wa chama cha Kabila, na hivi sasa anasubiri saini ya rais ili akabidhiwe rasmi ofisi.