Wampa ushauri huu
NA ABOUD MAHMOUD
WASANII na wanamichezo visiwani Zanzibar wamekipongeza Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa kumteua Dk. Hussein Ali Mwinyi kupeperusha bendera ya chama hicho kwa nafasi ya urais wa Zanzibar.
Wakizungumza na gazeti hili kwa nyakati tofauti walisema wanaimani kubwa na Dk. Mwinyi,kuwa mara baada ya kupata ridhaa ya wananchi wa Zanzibar, atafuata nyayo za Rais atakayeondoka madarakani Dk. Ali Mohammed Shein kwa kuwa karibu na wasanii na wanamichezo.
Walisema kwamba Dk. Shein amekuwa mstari wa mbele katika kusukuma gurudumu la wasanii na wanamichezo kwani wao ni kioo cha jamii katika mambo mbali mbali.
“Namuomba Dk. Mwinyi mara baada ya kupata ridhaa ya Wazanzibari asitusahau wasanii afuate nyayo za Dk. Shein, ambaye alikuwa na sisi bega kwa bega katika kufanikisha kazi zetu,”alisema Mwinyi Mpeku.
Mwema Khamis (Bi Njiwa) alisema ni vyema Dk. Mwinyi akipata nafasi ya kuiongoza Zanzibar, afuate nyayo za Dk. Shein kwani aliwafanyia mambo mengi mazuri wasanii .
Nae mwana michezo Salum Bausi Nassor alisema katika kipindi cha uongozi wa Dk. Shein sekta ya michezo iliimarika sana kwani aliweza kufufua michezo na kuendeleza mambo mbali mbali mazuri kupitia fani hiyo.