NA KHAMISUU ABDALLAH

MKURUGENZI Tume ya Taifa ya Uchaguzi NEC ofisi ya Zanzibar, Hamidu Mwanga amewasisitiza watendaji walioteuliwa kusimamia uchaguzi kuweka mbele suala la nidhamu na kuhakikisha uchaguzi mkuu hauingii dosari.

Amesema, NEC haitokuwa na muhali na kiongozi yoyote aliyepewa dhamana hiyo kusababisha uchaguzi kufutwa kwani wamewaamini kuona watasimamia suala hilo kwa uadilifu mkubwa.

Alisema, wasimamizi hao wana jukumu kubwa kuweka mbele suala la nidhamu na maadili ya kazi katika kipindi chote cha uchaguzi kwani jambo hilo ni la kitaifa.

“Yoyote atakaesababisha uchaguzi kufutwa basi atawajibika kufidia gharama zote za uchaguzi utakaofutwa hivyo wasidhani kwamba wameingia mkataba na NEC na watakapoharibu watakwenda nyumbani watawajibika kisheria,” alisema.

Alisema hayo wakati akizungumza na maofisa uchaguzi na wasaidizi wao katika majimbo mbalimbali ya Unguja katika ukumbi wa Sheikh Idrisa Abdulwakil Kikwajuni Mjini Unguja.

Alisema NEC iliwateuwa watu hao na kuamini kwamba wanaweza kusimamia jambo hilo kwa mujibu wa sheria na kuwapatia mafunzo ili kuweza kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi na kutimiza takwa la kisheria.

Aidha aliongeza kuwa watendaji hao wanatarajiwa kutumika kuwafundisha watendaji wengine watakaoteuliwa watakaofanya kazi katika vituo hivyo aliwashauri kuzingatia mafunzo wanayopatiwa.

Naye Hakimu wa Mahakama ya wilaya Mwanakwerekwe Suleiman Said Suleiman aliwasisitiza maofisa hao kuheshimu kiapo walichokula ili kujiepusha na makosa ambayo yanaweza kuwatia katika matatizo.

Alisema, kiapo walichokula ni muhimu, hivyo wanapaswa kuhakikisha hawafanyi makosa hasa ya kushabikia chama na kutoa siri kwani kufanya hivyo ni kosa la jinai.

“Kiapo hiki kinaweza kukubana wakati wote utakapofanya makosa, sipendelei kuona mtu yoyote anakwenda kinyume na kiapo hiki alafu mimi baadae nije kuwa shahidi mahakamani,” alisema.