NAIROBI, KENYA

WAHADHIRI  na wanachuo raia wa Kenya walioko Marekani wamekosoa vikali agizo lililotolewa na rais wa nchi hiyo, Donald Trump,la kutaka wanafunzi wote wa kigeni waondoke nchini humo ndani ya miezi miwili ijayo.

Profesa Kefa Otiso, mhadhiri raia wa Kenya katika Chuo Kikuu cha Bowling Green State alisema agizo hilo la Trump ni adhabu kali inayokusudia kuumiza.

Alisema hakuna kitu chochote kinachoweza kuhalalisha uvurugaji huo wa ghafla wa maisha ya Wakenya nchini Marekani.

Msomi huyo wa Kenya alisema sera za utawala wa Trump dhidi ya raia wa kigeni zinapaswa kuangaliwa, huku akiutaka ubalozi wa Kenya mjini Washington umwandikie barua ya malalamiko Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Mike Pompeo juu ya kadhia hiyo.

Kwa mujibu wa Rais wa Chama cha Wasomi wa Kenya, Jerono Rotich, kuna wanachuo zaidi ya elfu nne katika Vyuo Vikuu na taasisi za elimu ya juu nchini Marekani, katika mwaka wa masomo 2019/20.

Wanafunzi wa nchi mbali mbali walioko Marekani walikosoa vikali mpango huo wa Trump wa kuwafukuza nchini humo ndani ya miezi miwili ijayo.

Trump alisema iwapo vyuo hivyo havitofunguliwa ndani ya miezi miwili ijayo na masomo yakaendelea kwa njia ya Intaneti, basi serikali yake itawafutia wanachuo hao vibali vya kuendelea kuweko nchini humo.