NA HAJI NASSOR

WAFANYAKAZI wastaafu wilaya za Chake Chake na Mkoani, wanaopokelea penshini zao Mfuko wa Hifadhi ya Jamii Zanzibar (ZSSF), wamesema hatua ya kusogezewa vituo vya kufanya uhakiki hadi ngazi ya wilaya ni jambo jema.

Walisema katika miaka iliyopitia iliwalazimu kukusanywa pamoja kwenye jengo la ZSSF Tibirinzi, jambo ambalo lilisababisha usumbufu.

Wakizungumza na mwandishi wa habari hizi kwenye vituo vya uhakiki vya Mkoani na Chake Chake, walisema fikra iliyozaliwa na uongozi wa ZSSF wa kuwasogezea huduma hiyo wilayani mwao ni uamuzi mzuri.

Mmoja kati ya wastaafu hao, kutoka wizara ya afya, Omar Mjaka Ali, alisema sasa ZSSF imesikia kilio cha wastaafu kwa kubuni njia za kisasa za kuwaondoshea usumbufu.

Alieleza kuwa mbinu na busara za uongozi wa ZSSF za kuwafuata wastaafu hadi wilayani ndio ilikuwa kilio chao cha muda mrefu.

“Mimi kama msataafu lazima niupongeze uongozi wa mfuko, kwanza kwa kutuwekea vituo kwa mujibu wa maeneo yetu, jambo hili limeondoa foleni na kurahisisha zoezi la uhakiki,”alisema.

Nae Mwalimu msataafu wa skuli ya msingi Madungu, Bimdogo Said Suleiman, alisema alishangaa baada ya kufika kwenye meza ya muhudumu na kuchukuliwa alama za kidole na kumaliza zoezi kwa muda mfupi.