NA MWANAJUMA MMANGA

JESHI la Polisi mkoa wa Kusini Unguja limefanikiwa kuwakamata watu watano kwa matukio mbali mbali ikiwemo la udhalilishaji.

Kamanda wa Polisi Mkoa huo, Suleiman Hassan Suleiman, akiwataja watu hao ni Fauzia Ame Juma (22) mkaazi wa Uzi, Zakaria Mohammed Fumu (39) wa Bungi, Rehema Ernest (39) wa Jumbi, Febrona Paskal Saswenda (32) wa Kiboje na Salum Said Salum (47) mkaazi wa Tunguu.

Kamanda Suleiman, alisema mnamo Juni moja mwaka huu majira ya saa 5:00 za usiku huko Uzi, Fauzia alipatikana akiwa na nyongo 22 za bangi ambazo zinazoaminika kuwa ni dawa za kuleva yakiwa ni mafurushi mawili yaliyokuwa ameyahifadhi kwenye karatasi ya kaki.

Alisema vijana hao walipatikana kufuatia operesheni iliyofanywa ya kuwasaka wanaofanya biashra hiyo na uhalifu.

Tukio jengine limetokea Juni 5,  mwaka huu majira ya saa 10:00 za jioni Zakaria alipatikana akiwa na nyongo 129 za bangi zinazoaminika kuwa ni dawa za kulevya na ulevi wa kienyeji huko Bungi Wilaya hiyo.