LONDON, England

WATFORD wamemtimua kocha Nigel Pearson zikiwa zimesalia mechi mbili pekee kabla ya ligi kuu ya Uingereza (EPL) msimu huu kutamatika rasmi.

Sababu ya kufurushwa kwa Pearson ni matokeo duni ya kikosi hicho ambacho kwa sasa kinashikilia nafasi ya 17 na pointi 34, tatu pekee mbele ya Aston Villa na Bournemouth ambao pia wapo katika hatari ya kushushwa daraja mwishoni mwa kampeni za msimu huu baada ya Norwich City.

Pearson ambaye amewahi kudhibiti mikoba ya Leicester City, anakuwa mkufunzi wa tatu baada ya Javi Gracia na Quique Sanchez Flores kutimuliwa msimu huu huu.

Kocha wa vijana wasiozidi umri wa miaka 23, Hayden Mullins atasimamia mechi mbili za mwisho za Watford katika kipute cha EPL msimu huu dhidi ya Manchester City na Arsenal mtawalia. Atashirikiana na Graham Stack ambaye amekuwa msaidizi wa Pearson.