LONDON,UINGEREZA
SHIRIKA la kimataifa la kuwahudumia watoto, Save the Children; limesema kwamba janga la corona limesababisha hali ya dharura ya elimu ambayo haikutarajiwa.
Shirika hilo limeongeza kwamba takriban watoto milioni 9.7 wako katika hatari ya kutorudi skuli kuendelea na masomo, baada ya janga hilo kulazimisha skuli kufungwa.
Save the Children yenye makao makuu yake nchini Uingereza ilitoa taarifa kutoka katika shirika la Umoja wa Mataifa kuhusu Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO), iliyosema kwamba mnamo mwezi Aprili, takriban wanafunzi bilioni 1.6, ikiwa ni asilimia 90 ya wanafunzi ulimwenguni kote, walilazimika kuacha skuli.
Hatua hiyo ilitokana na masharti yaliyowekwa kuepusha kuenea kwa virusi vya corona.
Ilielezwa kwamba huenda ugumu wa kiuchumi, ukawatumbukiza kati ya watoto milioni 90 hadi milioni 117 katika umaskini.
Hata hivyo Mkuu wa shirika hilo Inger Ashing alizitaka serikali kuwekeza kwa dharura katika elimu.