NA ASIA MWALIM

JESHI la Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja, limewekamata watu 30 kwa tuhuma za kujihusisha na matukio mbali mbali ya kihalifu kwa kipindi cha Juni 3, hadi Julai 1, mwaka huu.

Kamanda wa mkoa huo, Awadhi Juma Haji, aliyasema hayo alipokuwa akizungumza na mwandishi wahabari hizi huko Ofisini kwake Mwembemadema Wilaya ya Mjini Mkoa wa mjini Magharibi Unguja.

Alisema matukio hayo ni pamoja na unyanganyi wa kutumia nguvu, uuzaji wa madawa ya kulevya, uvunjaji wa maduka ya miamala ya fedha na uvunjaji wa ofisi ya ulinzi shirikishi.

Alisema katika kupambana na uhalifu na wahalifu nchini, jeshi hilo limefanikiwa kuwakamata watuhumiwa watatu wanaohusika na matukio ya mara kwa mara ya unyanganyi wa kutumia nguvu, katika maduka yanayotoa miamala ya fedha katika maeneo mbali mbali ya mkoa huo.

Kamanda aliwataja wahusika hao ni Siya Katemi Tenera (41) mkaazi wa Kianga, Rajab Said Sonda (30) mkaazi wa Mwera Hawai na Ali Khamis Mbarouk (29) mkaazi wa Koani wilaya ya kati Mkoa wa Kusini Unguja.

Aidha katika tukio la uvamizi wa duka la dawa za binaadamu (Phamacy), alisema wahusika watukio hilo walivamia duka hilo linalomilikiwa na Abdulkadir Ismail Omar wakiwa na pingu walijitambulisha kuwa wao ni askari Polisi na kufanikiwa kuiba fedha taslimu kiasi cha shilingi 450,000.