NA LAYLAT KHALFAN

WAKALA wa Chakula, Dawa na Vipodozi Zanzibar, (ZFDA), imesema zoezi la ukamataji wa wafanyabiashara wanaouza maziwa katika chupa za plastiki ni endelevu.

Mkuu wa ukaguzi wa chakula Mohammed Shazil Shauri, aliyasema hayo ofisini kwake, Mombasa wakati  akizungumza na mwandishi wa gazeti hili.

Alisema tayari watu 10 wamekamatwa na kuchukuliwa hatua stahiki kwa kuwafahamisha utaratibu sambamba na kuyateketeza maziwa ambayo yamehifadhiwa katika chupa hizo.

Alisema ZFDA ilisitisha kuendelea na zoezi hilo kutokana na kuibuka ugonjwa wa maradhi ya corona, hivyo mamlaka hiyo haitasita kumchukulia hatua mfanyabiashara yeyote atakaebainika anakwenda kinyume na sheria.

Alisema wafanyabiashara wamefahamishwa madhara yatokanayo na chupa pale mtu anapoingiza maziwa moto na kwamba wapo walioelewa na kuahidi kubadilika.

Aliwataka wafanyabiashara wanaotumia chupa hizo kuacha mara moja kwa sababu madhara yake ni makubwa kuliko faida.

Aliwashauri wananchi kuachana na tabia ya kununua bidhaa kwenye chupa zilizotumika hususan maziwa kwa sababu sio salama.

Akizungumza kwa niaba ya wafanyabiashara wa maziwa katika maeneo ya Fuoni, Abdalla Said Kadar, alisema wapo tayari kutumia vifungashio vinavyotakiwa kwa ajili ya kuifanya biashara hiyo.

Alisema mbali ya hilo pia wanakabiliwa na  ukosefu wa jengo la kuuzia biashara hiyo na wanalazimika kuuza barabarani.