NA ABDI SULEIMAN
WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar, Mohamed Aboud Mohamed, ameelezea kuridhishwa na maendeleo ya ujenzi wa nyumba ya makazi ya Makamu wa Pili wa Zanzibar, inayojengwa Pagali wilaya ya Chake Chake, Pemba.
Ujenzi huo unaendelea kwa hatua za mwisho ambapo kwa sasa nyumba hizo ziko katika hatua ya kuwekewa madirisha na kutengeneza eneo la kuingilia.
Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kukagua ujenzi huo, alimtaka Mhandisi wa ujenzi wa nyumba hiyo pamoja na wakala wa majengo Pemba, kuhakikisha nyumba hiyo inakabidhiwa serikalini mwezi Septemba mwaka huu.
“kwa sasa hali ya ujenzi imefikia hatua nzuri, kilichobakia ni wakandarasi kukamilisha sehemu iliyopo ikiwa bado kama hamujapewa pesa zenu semeni ili ujenzi ukamilike kwa wakati,”alisema.
Alisema bado nia ya serikali kujenga nyumba za viongozi bado iko pale pale, kwanza imeanza na nyumba hiyo huku ikitarajiwa kuendelea na maeneo mengine.
Akizungumzia nyumba za maafa Tumbe, pia alimtaka mkandarasi wa ujenzi wa nyumba hizo kuhakikisha anazidisha nguvu ili nyumba 15 za awamu ya kwanza ziweze kukabidhiwa serikalini na kupatiwa wananchi.
Alisema itakuwa ni jambo la faraja kwa nyumba hizo kufunguliwa na Dk. Shein kabla ya muda wake haujamaliza kwani nyumba za awamu ya pili zitafunguliwa na kiongozi anayefuata.
“Kwa sasa hali ya ujenzi wa nyumba hizi unaridhisha, nyumba 11 tayari hizo nne zilizobakia mjitahidi zikamilike kabla ya Septemba pamoja na msikit, skuli na maduka,”alisema.