NA SABIHA KHAMIS, MAELEZO

WAZIRI wa Afya, Hamad Rashid Mohamed amelishukuru shirika la Afya Duniani (WHO) kwa juhudi kubwa walizozichukuwa kushirikiana na serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika mapambano dhidi ya maradhi ya corona nchini.

Waziri huyo alieleza hayo huko ofisini kwake Mnazi Mmoja wakati akizungumza na mwakilishi mkaazi wa WHO, Dk. Andemichael Ghirmy alipofika ofisini hapo kujua hatua iliyofikia Zanzibar katika kukabiliana na maradhi.

Waziri huyo alibainisha kuwa maradhi hayo yamedhibitiwa kwa kiasi kikubwa hali ambayo imewapa matumaini mazuri kiasi cha kuruhusu shughuli za kikazi kuendelea kama kawaida na kuruhusu wageni wakiwemo watalii kuingia nchini.

“Tumeruhusu wageni waingie nchini bila ya wasiwasi wowote kwani tumejipanga vizuri kwa matibabu na kuwashughulikia kwa kuwapima na kujua taarifa zao… Zanzibar corona imepungua kwa kiasi kikubwa na ikigundulikana mmoja wao ana maradhi tutahakikisha tunampatia matibabu”, alisema waziri huyo.

Waziri huyo alilipongeza Shirika hilo kwani udhibiti wa maradhi hayo unatokana na juhudi za pamoja kwa kutoa misaada yao na kupeana taarifa za kitaalamu.

Hata hivyo, aliwataka wananchi kuchukua tahadhari kwa wageni wanaoingia kwani bado zipo nchi za jirani zinaendelea kusumbuliwa na maradhi hayo.

Aliwataka washirika wa kimaendeleo kuendelea kuwaunga mkono mara tu inapotokea mripuko wa maradhi ya aina yoyote ikiwemo kipindupindu, malaria na maradhi mengineyo ili kuyadhibiti kwa haraka.

Hata hivyo, waziri huyo alifanya ziara kutembelea katika maabara akiwa na mwakilishi mkaazi huyo wa WHO katika hospital ya Rufaa Mnazi Mmoja kuona kifaa cha kupimia corona.

Naye Mwakilishi wa Shirika la Afya Duniani, Dk. Andemichael Ghirmy alisema ataendelea kushirikiana na serikali kupitia wizara ya afya na kuhakikisha wanakwenda sambamba na maradhi ya miripuko yatakayojitokeza.