YAMOUSSOUKRO, IVORY COAST

WAZIRI  Mkuu wa Ivory Coast, Amadou Gon Coulibaly, amefariki dunia ghafla usiku wa kuamkia jana akiwa na umri wa miaka 61.

Shirika la habari la IRIB limeripoti habari hiyo na kumnukuu Rais Alassane Ouattara wa Kodivaa akitangaza kwamba Ivory Coast iliingia kwenye msiba wa kuondokewa ghafla na Coulibaly.

Aidha alisema,Waziri Mkuu Coulibaly alishiriki kwenye kikao cha kila wiki cha Baraza la Mawaziri la serikali ya Kodivaa, hali yake ikawa mbaya na amefariki dunia hospitali.

Mwezi Machi mwaka huu, Coulibaly aliteuliwa na chama tawala cha Ivory Coast kugombea urais kwa tiketi ya chama hicho ili kumrithi Rais Alassane Ouattara.

Waziri Mkuu huyo alirejea nchini Kodivaa tarehe pili mwezi huu wa Julai baada ya kupitisha muda mrefu wa matibabu nchini Ufaransa,aliwahi kufanyiwa operesheni ya moyo mwaka 2012.

Ouattara alimtaja Colibaly kwamba alikuwa mtu wake wa karibu mno katika kipindi cha miaka 30 iliyopita.

Wakati Waziri Mkuu Coulibaly alipokuwa anaendelea na matibabu nchini Ufaransa, Waziri wa Ulinzi wa Kodivaa, Hamed Bakayoko ndiye aliyesimamia ofisi ya Waziri Mkuu wa nchi hiyo kwa muda wa miezi miwili.

Uchaguzi ujao nchini Ivory Coast unahesabiwa kuwa ni mtihani wa kupima utulivu na amani katika nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika yenye historia ya machafuko ya uchaguzi.