KINSHASA,DRC

WAZIRI wa Sheria wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo Celestin Tunda amejiuzulu baada ya kuzozona na rais wa nchi hiyo kuhusu sheria zilizopendekezwa ambazo zitawapa wanasiasa udhibiti wa mashitaka ya jinai.

Katika taarifa ya kujiuzulu,Tunda hakutaja sababu ya kujiuzulu kwake.

Waitifaki wa kisiasa wa Tunda walikuwa wanataka wizara ya sheria iwe na uwezo mkubwa zaidi wa kusimamia idara ya mahakama nchini humo.

Hatua ya Tunda kujiuzulu inaashiria msuguano katika serikali ya mseto baina ya Rais Felix Tshisekedi na rais aliyemtangulia Joseph Kabila.

Tunda ni waziri wa kwanza kujiuzulu katika serikali, ambayo ilichukua miezi minane kuundwa na hatimaye kutangazwa Agosti mwaka jana.

Peter Kazadi wa chama cha UPDS cha Rais Tshisekedi alisema Tunda alituma barua katika bunge kuhusu mabadiliko ya mfumo wa sheria bila kushauriana na serikali.

Alisema waziri huyo alikiuka taratiabu zilizowekwa na kwa msingi huo kujiuzulu kwake ni jambo lililotarajiwa.

Hali ya taharuki ilitanda mwezi Juni wakati Tunda alikamatwa kwa muda mfupi na akaachiliwa huru baada ya Waziri Mkuu Sylvestre Ilunga kutishia kuwa serikali itajiuzulu.