NA MWANDISHI WETU

WANAWAKE vijana wanaoishi katika umasikini wamefanikiwa kujikwamua Katika maisha magumu baada ya kujiunga na vikundi vya kuweka na kukopa, ambapo kwa pamoja wameweka akiba ya jumla ya shilingi 116.5 milioni  kuanzia Juni mwaka jana.

Wanawake hao wako katika mpango kuwawezesha wanawake kiuchumi Zanzibar (WEZA III) unaotekelezwa na TAMWA-Zanzibar ambao unawanufaisha wanawake 1,207 kati yao 694 wako kisiwani Pemba.

Mkurugenzi wa TAMWA-Zanzibar, Dk. Mzuri Issa Ali, alisemwa wanawake hao wako katika shehia 24 Unguja na Pemba.

Mzuri alisema fedha hizo zimekusanywa kupitia mpango wao wa kukutana kila wiki ambapo mwanachama huweka kati ya shilingi 500 hadi 10,000 na kufanya biashara mbali mbali zinazowaingizia kipato.

Alisema wanawake hao kuanzia miaka 18 hadi 40 walichaguliwa kuingia katika mpango huo kutokana na kutojishughulisha na biashara yoyote na kutokua na kipato chochote.

Alisema kijiji cha Mkanyageni, wilaya ya mkoani Pemba ni moja kati ya eneo la mpango huo ambalo lina vikundi hivyo na kwa pamoja wanawake wamefanikiwa  kuweka shilingi 3.5milioni.

Mwenyekiti wa kikundi cha Maisha Siri, Hadia Hashim Awesu, alisema kuwepo vikundi vya aina hiyo kumesaidia kuwainua wanawake ambapo hadi mwaka hana wanawake wenzake walikuwa hawajishughulishi na kazi yoyote ya kipato.

Alisema baada ya kupata mafunzo walianza na kilimo cha mboga na baadae kuzalisha sabuni, mafuta, majani ya chai, ukulima wa vanila na ufugaji kuku.

“Mpaka sasa tumeweka akiba ya jumla shilingi 3.5 milioni kupitia uwekaji wa hisa ambapo mtu mmoja huweka kati ya shilingi 2,000 hadi 10,000 kwa wiki,” alisema.

Aidha aliongeza kwamba kikundi kimefanikiwa kununua banda kwa ajili ya ufugaji kuku lenye thamani ya shilingi 1.5 milioni.

“Tulianzisha biashara ya kuuza kuni kwa ajili ya kuongezea mtaji wetu na kupitia shughuli hizo tumefanikiwa kununua kiwanja na banda la kuku kwa shilingi 1.5 milioni ambapo tunataka kuwezeka ili tukuze ufugaji,” aliongeza.

Fatma Mohamed Juma, mwanachama wa kikundi hicho, alisema licha ya maendeleo ya pamoja lakini pia kikundi kimemsaidia kuinuka kiuchumi kwa mwanachama mmoja mmoja kupitia uchukuaji wa mikopo kwenye mfuko wa hisa.

“Nilipoingia kwenye kikundi nilikopa shilingi 300,000 kwa ajili ya kununua cherehani, nashukuru imenisaidia kukuza kazi yangu ya ushonaji na mpaka sasa natarajia tena kukopa pesa nyingine ili niongezee kununua charahani nyingine ya kisasa kwani wateja wameongezeka,” alisema.

Kwa upande wake, Bijuma Khamis Kombo, kutoka kikundi cha Safinia kilichopo shehia ya Majenzi Micheweni, alisema vikundi hivyo ni mkombozi kwa wanawake wengi katika eneo lao.

Alisema amefanikiwa kununua pikipiki ambayo inamuingizia kiasi cha shilingi 60,000 kwa mwezi.

Mradi wa WEZA III unatekelezwa na Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake TAMWA- Zanzibar kwa kushirikiana na Zanzibar Milele Foundation.