USWISI, GENEVA
SHIRIKA la afya duniani WHO limetangaza kuwa linaunda jopo huru ili kuchunguza jinsi lilivyoshughulikia janga la Covid-19.
Mkurugenzi Mkuu wa WHO Tedros Adhanom Ghebreyesus aliuambia mkutano wa wawakilishi 194 wa WHO uliofanyika kwa njia ya mtandao, kuwa Waziri Mkuu wa zamani wa New Zealand Helen Clark na aliyekuwa rais wa Liberia Ellen Johnson Sirlef walikubali kuongoza jopo hilo na pia kuchagua wanachama wake.
Tedros alisema kuwa huu ni wakati wa kutafakari na kuyaelezea mataifa wanachama wa shirika hilo kuwa walikubaliana kwa kauli moja mnamo mwezi Mei kutathmini jinsi shirika hilo la Umoja wa Mataifa lilivyoshughulikia janga la virusi vya Corona. Utawala wa rais Donald Trump nchini Marekani, ulikosoa shirika hilo kwa namna lilivyoshughulikia janga hilo, na wiki hii umemuandikia barua katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres, kumuarifu juu ya uamuzi wake kujitoa katika shirika hilo mwaka ujao.