NA KAUTHAR ABDALLA

WIZARA ya Kazi,Uwezeshaji,Wazee,Wanawake na Watoto inafanya kila jitihada  kuhakikisha inapunguza kiwango cha ukosefu wa ajira nchini.

Mkurugenzi wa  Usalama na afya Kazini, Suleiman Khamis Ali, amesema jitihada hizo ni kusimamia utekelezaji wa mpango wa ajira kwa vijana na kupanua program za uwezeshaji wananchi kiuchumi.

Mkurugenzi alisema hayo kwa niaba ya Waziri wa Kazi, Uwezeshaji, Wazee, Wanawake na Watoto, Moudline Castico, katika ufunguzi wa mafunzo ya wadadisi ya utafiti wa watu wenye uwezo wa kufanya kazi wa mwaka 2020/21,yaliyofanyika katika Ofisi ya Mtakwimu mkuu wa Serikali Mazizini.

Alisema utafiti wa mwisho wa watu wenye uwezo wa kufanya kazi ulifanyika mwaka 2014, ambapo matokeo ya utafiti huo yalionesha kiwango cha watu wasio na ajira kilikuwa ni asilimia 14.3, kiwango ambacho ni kikubwa Zaidi kwa maeneo ya mijini kikiwa na asilimia 23.3 ikilinganishwa na maeneo ya vijijini asilimia 7.5.

Alifahamisha kuwa taarifa za utafiti huo zitatumika katika utayarishaji wa dira mpya ya maendeleo ya Zanzibar ya 2050, mpango wa muda mfupi wa utekelezaji wa dira ya 2050,utekelezaji na tathmini ya mpango wa malengo endelevu ya maendeleo na ajenda ya Afrika ya 2063.