NA MAULID YUSSUF, WEMA

WIZARA ya Elimu na Mafunzo ya Amali, imekataa kusaini fomu ya makabidhiano ya majengo yalio chini ya mkandarasi Salim Constructors LTD yaliyopo wilaya ya Kati na Mkoa wa Kusini Unguja kutokana na kutomalizika kwa baadhi ya miundombinu.

Akizungumza katika majumuisho ya ziara ya kuangalia majengo ya maabara za sayansi ‘school hubs’, kwa skuli nne zinazosimamiwa na mkandarasi huyo, Katibu Mkuu wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali, Dk. Idrisa Muslim Hija amesema  makubaliano yao ni kukabidhiana majengo yote na endapo jengo moja litakuwa na kasoro hawatoweza kusaini fomu ya makabidhiano yao.

Alisema ni utaratibu wa Wizara yake kupokea majengo yakiwa yamekamilika yakiwa na miundombinu yote kama walivyokubaliana na sio moja moja.

Dk. Muslim alifahamisha katika ziara yao wamebaini kujitokeza tatizo la umeme katika ‘school hubs’ ya Uroa hali inayosababisha kushindwa kukagua mifumo yote ya umeme iliyomo kwenye maabara hiyo.

Aidha alisema ili taifa lizalishe wasomi hasa wa masomo ya sayansi ipo haja ya kuboresha miundombinu bora ya kielimu kuanzia majengo pamoja na maabara za kutosha.

Hata hivyo, aliwahimiza wakandarasi kufanya marekebisho madogo madogo yaliyojitokeza katika majengo hayo kwa wakati waliokubaliana. 

Naye Mkurugenzi Idara ya Mipango Sera, Khalid Masoud Waziri alisema lengo la ziara hiyo ni kuhakikisha majengo yote ya mradi wa ujenzi wa maabara za kisayansi yanakamilika kwa kiwango imara na salama kwa ajili matumizi ya watoto wao.

Kwa upande wake mshauri elekezi wa mradi huo Casmil Ntobangi alisema ukosefu wa mchanga, mvua kubwa na mripuko wa maradhi ya covid 19 vimesababisha kuchelewa kukamilika kwa wakati maabara hizo.