TEHRAN,IRAN

MSEMAJI wa Wizara ya Afya, Tiba na Mafunzo ya Utabibu ya Iran amesema hadi sasa watu 242,351 walioambukizwa virusi vya corona wamepata nafuu na kuruhusiwa kutoka hospitali.

Sima Saadat Lari alithibitisha kutambuliwa kesi mpya 2,625 za maambukizi ya corona katika muda wa masaa 24 yaliyopita na kueleza kuwa, hadi sasa watu 278,827 waliambukizwa corona  Iran kwa mujibu wa vigezo vya wazi vya utambuzi.   

Lari alisema kufariki dunia watu 229 katika muda wa masaa 24 na kuongeza kuwa, idadi ya watu waliokufa kutokana na maambukizi ya virusi vya corona nchini Iran imefika elfu 14 na 634.  

Wakati huo huo idadi ya watu walioambukizwa virusi vya corona duniani ni zaidi ya milioni 14 na 880,000.

Watu wasiopungua 613,000 miongoni mwa idadi hiyo tajwa ya maambukizi walifariki na wengine karibu milioni nane na 935,000 walipata nafuu na kuruhusiwa kutoka hospitali.  

Katika jitihada za kutokomeza ugonjwa wa Covid-19, makundi mengi ya utafiti nchini Iran yanafanya kazi ya kuzalisha chanjo ya ugonjwa wa Covid-19 .

Akihojiwa wiki hii kuhusu mafanikio hayo ya kiuatafiti, Daktari Saeed Namaki, Waziri wa  Afya, Tiba na Mafunzo ya Utabibu wa Iran alieleza matarajio yake kuwa siku chache zijazo watawatangazia wananchi habari njema kuhusu jambo hilo.