ZAZPOTI

CHAMA cha Soka Wilaya ya Mjini (ZFA), kimeshauriwa kuifuta ligi daraja la pili na kuanza maandalizi ya msimu ujao ili wachezaji waweze kujipanga vizuri zaidi.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi,Kocha Mkuu wa timu ya Puling Land inayoshiriki ligi hiyo,Yussuf Saleh ‘Lule’, alisema, ni vyema ligi hiyo kusitishwa kwani wachezaji wengi hawana kiwango kutokana na kukosa mazoezi.

Alisema kwamba muda uliobakia ni mfupi na wachezaji hawajafanya mazoezi kwa muda mrefu jambo ambalo litashusha hadhi ya ligi hiyo.

“Naiomba ZFA kuifuta ligi kwa sababu wachezaji hawapo vizuri kimazoezi na gharama kubwa za uendeshaji wakati hali ya maisha ni ngumu”, alisema.
Kocha huyo, alisema, mazoezi ni jambo bora kwa mchezaji ili afanye uzuri na kutoa mfano kwa timu zinazoshiriki Ligi Kuu ya Zanzibar kuonekana zikiboronga kutokana na kutokua na mazoezi ya kutosha kabla ya kurudi uwanjani.

“Kwa upande wa timu yangu haina mazoezi na mpaka hivi sasa bado hatujajua tutaanza lini, lakini, jambo hili sio kwetu sisi tu hata wenzetu nao wapo kama sisi”.
Hivyo, alisema, endapo ZFA itafanya uamuzi huo watakua wamefanya jambo bora kwani hivi sasa viongozi na wachezaji wamekua wakiangalia msimu ujao wa ligi na sio uliobakia.