NA MWAJUMA  JUMA

SHIRIKISHO la Soka Visiwani Zanzibar limefuta matokeo ya mechi nne za ligi kuu ya Zanzibar, baada ya kubaini upangaji wa matokeo.

Michezo iliyofutiwa matokeo hayo ni mchezo nambari 234 uliowakutanisha Mafunzo na Jang’ombe Boys, mchezo nambari 243 kati ya KMKM na Jamhuri, Mchezo nambari 244 ulikuwa kati ya Chuoni na Mwenge na mchezo nambari 237 kati ya Malindi na Jamhuri.

Kwa mujibu wa barua zilitolewa na Kamati ya kusimamia mashindano na ligi ya Shirikisho hilo, ambazo zimetiwa saini na katibu wake Hussein Ahmada, mbali na kuyafuta matokeo hayo lakini pia imezipiga faini ya shilingi milioni 1 kila mmoja.

Michezo ya ligi hiyo ilichezwa kwa wakati na siku tofauti ambapo Jamhuri imepigwa faini mara mbili kwa mchezo kati yake na KMKM iliyofungwa mabao 7-0 na mchezo kati yake na Malindi ambapo ilifungwa mabao 7-0.

Kwa upande wa timu ya Mwenge nayo ilicheza na Chuoni na kufungwa mabao 3-0 wakati Jang’ombe Boys na Mafunzo zimefutiwa matokeo yao baada ya kutoka sare ya kufungana mabao 2-2.

Kwa mujibu wa barua hizo faini hizo zimetakiwa kulipwa si zaidi ya  wiki moja ya barua hiyo, na kusisitiza kuwa ZFF haitosita kuchukuwa hatua za kinidhamu kwa timu yoyote itakayoshiriki katika kitendo cha upangaji wa matokeo.