Ataka kuchaguliwa viongozi bora na sio bora viongozi

NA MADINA ISSA

IKIWA kipenga cha uchukuwaji wa foma za wagombea mbalimbali wa nafasi za uongozi ndio tayari kimepulizwa jamii na wananchi kwa ujumla wametakiwa kuwachagua viongozi bora na sio bora viongozi.

Mjumbe wa Kamati kuu ya Halimashauri kuu ya Chama cha Mapinduzi (CCM) Taifa, ambae pia ni Makamu was Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, amewataka wananchi kutofanya makossa wa kuwachagua viongozi wao hasa wa mmajimbo.

Katika ziara yake ya kichama katika mikoa minne ya Chama cha Mapinduzi (CCM) Unguja aliyoifanya hivi karibuni ilioanza Juni 30 hadi Julai 2 mwaka huu ilikuwa na lengo kuweka mikakati ya kuona ushindi wa uchaguzi mkuu wa mwaka 2020 unapatikana kwa vishindo.

Aliwataka wanaCCM kuhakikisha kuwa viongozi wanaowachagua watajali wajibu wa waliowachagua kwa kuweza kuwatekelezea huduma za kimaendeleo katika majimbo yao.

Pamoja na mambo mengine, katika ziara hiyo, Makamo Rais Samia aliweza kukutana na wajumbe wa Halmashauri za Mikoa hiyo, kwa lengo la kuimarisha Chama cha Mapinduzi, pamoja na kujua matayarisho ya Uchaguzi ikiwa kimkoa wamejipanga vipi na matayarisho na mikakati ikoje katika mikoa ambapo ni kiasi gani wamejipanga ili kuona ushindi unakuwa mkubwa katika Uchaguzi unaotarajia kufanyika baadae mwaka huu.

Ziara hiyo pia ilitoa hamasa kubwa katika kwa watendaji na wanachama wa CCM kwani waliweza kutoa maazimio yao muhimu ambayo yataweza kuwasaidia kuibua ushindi Mkuu wa 2020.

Mama Samia amekuwa na sifa za kutoa ushauri katika ziara hiyo, ambapo viongozi walikuwa wakimpongeza na hata kumuahidi kuendeleza ushauri wake aliyokuwa akiutoa iliwa na lengo la kuimarisha chama pamoja na kupatikana ushindi katika Chaguzi na kuendelea kushika dola.

Katika ziara hiyo, Mama Samia ameonesha mwanga kwa wajumbe wa halmashauri hiyo kwa kuona wanapata viongozi waliokuwa bora na sio bora kiongozi katika majimbo na kuachana na tabia ya kukinunia chama endapo wanachama kaomba ridhaa na hakushinda katika teuzi za ndani ya chama.

“Chama chetu hakina sifa ya ubaguzi wala ubinafsi sote tunapogombea na majina yakitolewa tusinune na tuendeleze mapambano ili ushindi upatikane mapema” anasema mjumbe huyo wa kamati kuu ya Halmashauri Kuu ya Chama.

Aliendelea kuwakumbusha wajumbe hao kuwa uongozi wowote unatokana na kujitolea katika chama pamoja na kuleta maendeleo kwa vitendo ikiwa kiongozi pamoja na kuwakumbusha kuwa Mungu ndie pia anayesimamisha kuwa kiongozi na sio mtu mwengine.

Katika mikutano yake hakusita kuwakumbusha wajumbe hao kuwa na utayari ya kuwachagua viongozi watakaoweza kuwaletea maendeleo wananchi wao kwa mujibu wa ilani ya chama pamoja na ahadi wanazozitoa.

Ziara yake ilioanzia Mkoa wa Kusini Unguja na kukutana na viongozi wa halmashauri kuu ya Mkoa na kuwataka kuendeleza umakini katika kupitisha wagombea na kuwataka kuzingatia kanuni za uteuzi wa wagombea uongozi katika vyombo vya dola, ikiwemo uongozi na maadili.

Alisema katika Kamati za siasa kumeonekana kuwa zimekuwa zikiwapitisha wagombea na baadaye wanapokuja katika nafasi za uongozi na kutowajibika wanalalamika kwa kudai kuwa hawaonekani majimboni na hawawajibiki jambo ambalo halitakiwi katika chama ambapo limekuwa likipelekea kutotekeleza ilani ya chama hicho kwa vitendo na kukirejesha nyuma Chama.

“Mkishawapitisha hao wagombea ambao wanatumia fedha mnaanza kulalamika tangu aingie amelitupa jimbo ndio kaja mara hii lakini hawa watu mnawapitisha wenyewe na sisi huku juu mmetuletea na alama nzuri tunasema hawa ndio wanaoaminika kwenye kamati zao warudisheni hivyo muwe makini katika upitishaji wenu wa viongozi,”anasema.

Makamu wa Rais amewataka wajumbe hao wajipange vizuri katika kupitisha wagombea watakaowania nafasi mbalimbali kufuata miongozo ya kanuni za uteuzi wa kugombea uongozi katika vyombo vya dola na katiba ya chama katika kuwapata wagombea.

Alisema kwa kuzingatia miongozo hiyo itasaidia kuwapata wagombea wenye sifa za kuwatumikia wananchi na kwamba kufuata misingi hiyo ni vigumu sana kuwapata wagombea ambao wanaotumia rushwa ndani ya chama.

Katika maelezo yake mama Samia alisema kwa mujibu wa kanuni hizo zimeweka wazi namna ya kuwapata wagombea na namna ya kutoa alama kwa wagombea hao na kwamba vitabu hivyo vya kanuni ni muhimu sana hasa kwa wakati huu.

“Kama mnamjadili mgombea mnatakiwa mtafute vitabu hivi msome mvijue ili mukiingia kwenye hiyo ya kazi mjue mnafanya nini mara nyingi kinachofanyika kuwa wanarusha tu alama ninachowaomba msiharibiane sifa wala msipe sifa aliyekuwa hana sifa kugombea ni haki ya kila mtu,”aliwakumbusha wajumbe hao.

Mbali na hilo, Makamu huyo wa Rais aliwataka wajumbe hao kuacha kuwabeba wagombea katika uchaguzi wa ndani, kwani watakuja kuoneana aibu kutokana na kuwa wanaweza kumbeba mgombea na kuahidiwa vitu vingi.

“Muacheni kila mtu ahangaike kwa uwezo wake wakati wa kampeni zikiruhusiwa msibebane mtakuja kuoneana aibu,”alisema

Kwa pamoja wajumbe hao wameonekanwa kutoka na maazimio ya kuendeleza ushirikiano katika mikoa yao na kuahidi kuwa ushindi utapatikana kwa asilimia kubwa kuliko miaka yote ya uchaguzi uliofanyika Tanzania.

Wajumbe hao walisema kuwa wamejipanga kimkakati katika kuhakikisha majimbo yote yanakwenda CCM katokana na kuwa upo mipango imara na kuwa na sera nzuri katika chama hicho.

Walisema uongozi wa mkoa huo wamejipanga kwa kushirikiana na makundi mbalimbali ya Jumuiya za chama ili kujipanga yema kwa ajili ya uchaguzi mkuu kwa lengo la kuipatia ushindi wa kishindo CCM.

Kwa mantiki hiyo basi ipo haja kwa wananchi kuona kuwa wanachagua viongozi wao ambao watawaletea maendeleo kwani kufanya hivyo kutawawezesha kufikia lengo lililokusudiwa.

Kwa pamoja inawezekana kabisa kila mmoja iwapo atatizmiza wajibu wake kwa maendeleo ya taifa.