NA MARYAM HASSAN
KIKOSI cha Zimamoto na Uokozi Zanzibar (KZU) kimeipongeza serikali ya awamu ya saba ya Dk. Ali Mohmmed Shein kwa kuwapatia vifaa vya uokozi baharini.
Hayo yameelezwa na Naibu Kamishna wa kikosi hicho Gora Haji Gora wakati akizungumza na Zanzibar leo huko Ofisini kwake Kilimani Mjini Unguja.
Alisema kitendo kilichofanywa na Dk. Shein cha kuwapatia boti ya uokozi ya kisasa (Fire Master One) kutapunguza majanga ya baharini.
Naibu huyo alieleza kuwa boti hiyo ina uwezo wa kukimbia kwa kasi ili kulifikia eneo la tukio na kufanya uokozi kwa haraka sana, jambo ambalo limewapa faraja.
Pia alifahamisha kuwa boti hiyo ina uwezo wa kuokoa watu 50 kwa wakati mmoja na kuwafikisha sehemu husika kwa ajili ya kupatiwa huduma.
Alieleza kwamba majanga kama ya moto wa aina zote ikiwemo gesi na mafuta yatafikiwa kwa haraka kwa lengo la kuokoa mali zilizokuwemo katika chombo husika.
Aidha alisema boti hiyo itaweza kutoa huduma kwa ufanisi na kuvifikia visiwa vyote vya Unguja na Pemba.
Gora alieleza kwamba apo awali kikosi chao kilikuwa hakina boti ya uokozi na kulazimika kushirikiana na kikosi cha KMKM kwa ajili ya kutoa huduma za uokozi pindi majanga yanapotokea.