Mabodi ataka wenye malalamiko wakate rufaa

Asema mizengwe ikithibika kanuni ‘kupindua meza’

KHAMISUU ABDALLAH NA ASYA MWALIM

CHAMA cha Mapinduzi CCM Zanzibar, kimesema aliyekuwa hakuridhika kwenye zoezi la kura za maoni zilizofanyika juzi la kuwachagua wagombea wa ubunge na uwakilishi wawasilishe malalamiko kwenye chama hicho ndani ya kipindi cha saa 24.

Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Dk. Abdulla Juma Sadalla alieleza hayo jana wakati akitoa taarifa kwa vyombo vya habari ofisini kwake Kisiwandui mjini Zanzibar.

Dk. Mabodi alisema kwa mujibu wa kanuni ya chama ya uteuzi wa wagombea na uongozi katika vyombo vya dola ukurasa wa 35, umeeleza utaratibu wa kushughulikia malalamiko na kuwataka waliobaini kwamba kuna mambo hawakuridhika nayo kuitumia fursa hiyo.

Naibu huyo alibainisha kuwa kukaa kimya kwa makada waliokuwa hawakuridhika na mchakato huo hakutasaidia na itakuwa wamepoteza fursa ya muhimu ya kudai haki zao na kwamba makosa yakibainika yanaweza kukiathiri chama.

Alifahamisha kwamba kamati za siasa katika kanuni hiyo zimelazimishwa kushughulikia malalamiko na ikithibitishwa inatakiwa itoe maamuzi au kupeleka katika ngazi za juu na maoni yake kusikilizwa.

“Tunavyo vyombo vyetu vya nidhamu na udhibiti na vyombo vya usalama na maadili ambavyo vinafanya kazi chini kwa chini na tumepeleka mapendekezo kwani masuala ya rushwa ni masuala ya kitaifa ambapo ZAECA na polisi wanashughulikia masuala ya kisheria yote”, alisema. 

Akizungumzia suala la rushwa linalolalamikiwa katika zoezi hilo la kura za maoni, Dk. Mabodi alisema ofisi yake haina taarifa za kuwepo kwa malalamiko hayo.

“Mpaka sasa tupo shuwari kuna wanachama tu ambao hawajaridhika inawezekana kwamba wanasema ukweli au mbinu ya kupakana matope wapo ambao hawakufurahika hivyo chama chetu kina misimamo mizuri ya kutatua matatizo yake kwa kufuata kanuni”, alisema.