NA KHAMISUU ABDALLAH, DAR ES SALAM

BODI ya Mapato Zanzibar (ZRB), imeshauriwa kuanzisha matawi yake kila mikoa, ili kurahisisha upatikanaji wa huduma.

Ushauri huo umetolewa na wananchi mbali mbali wanaotembelea banda ya bodi hiyo katika maonesho ya 44 ya kimataifa sabasaba yanayofanyika jijini Dar es salam.

Walisema, bodi ikiweza kuanzisha vituo hivyo basi kwa kiasi kikubwa itawarahisishia wafanyabiashara kufata huduma makao makuu ya bodi hiyo.

Ahmada Yussuf, alisema kwa kiasi kikubwa wameweza kutambua baina ya ZRB na TRA kwani walikuwa wakitambua kuwa chombo hicho ni kimoja katika ukusanyaji wa mapato. 

Joseph Muhinda, aliishauri bodi hiyo mbali na kutoa elimu  ya kodi pekee katika maonesho hayo,  ni vyema kutoa huduma zake ikiwemo utoaji wa leseni za udereva, pamoja na usajili wa vyombo vya moto.

Nae, Jaji Agoza Mwipopo, aliiomba serikali kuanzisha kituo kimoja ambacho kitakuwa kinasimamia kodi zote kwa upande wa Zanzibar, ili kuepusha changamoto kwa wafanyabiashara.

Nae, Ofisa Uhusiano ZRB, Badria Attai Masoud, alisema maonesho kwa mwaka huu yameleta mafanikio makubwa ukilinganisha na yaliyopita kwani wananchi wengi walikuwa wakihoji baina ya ZRB na TRA kuwa ni tasisi moja ya ukusanyaji wa kodi.

Alisema, mpaka sasa zaidi ya wananchi 210 wametembelea katika banda hilo na kupata elimu juu ya huduma mbalimbali zinazotolewa na bodi hiyo.

Hivyo, aliwaomba wafanyabiashara kutumia fursa mbali mbali za kufanya biashara zake Zanzibar, na uwekezaji kwani serikali imekuwa ikiwajali wafanyabiashara wake ikiwemo kupunguza kodi na kufuta tozo ambazo hazina ulazima kwa wananchi wake.