ASSALAMU ALAYKUM wapendwa wasomaji wangu wa safu hii. Ni Jumapili nyengine ambayo tumebarikiwa na Mungu kukutana tena na kujuzana mambo mazuri yanayohusu namna ya kujenga mahusiano yetu.

Leo tutaangalia mambo ambayo hutumika kama kigezo cha kupima uaminifu na upendo wa kweli kwa wanandoa.

Maana yangu ni kwamba, sio wote waliopo kwenye ndoa huwa na sifa ya uaminifu na upendo wa kweli kwa wenziwao.

Wengine huingia kwenye ndoa na kimuonekano wakaonekana na sifa zote hizo mbili, lakini kinyume chake wanaigiza tu na inahitaji muda kuwagundua.

Yawezekana ikawa sio rahisi kuyatambua makucha waliyoyaficha, hii ni kutokana na muendelezo wa maisha ya kawaida munayoishi ambayo bado hayajakumbwa na changamoto yoyote.

Mume au mke mkweli aliyemuaminifu na mwenye upendo wa dhati kwa mwenziwe utamjua. Kwanza siku zote huwa si muigizaji na anachokifanya kimatendo huwa anamaanisha.

Vifuatavyo ni vigezo muhimu vinavyopima uaminifu na upendo wa kweli kwa wanandoa.

MARADHI / UGONJWA

Hichi ni kigezo namba moja cha kumjua mwenza wako namna alivyo kwako. Ugonjwa niliokusudia hapa sio ule wa kawaida wa kuumwa siku mbili tatu baadae ukapoa na kurudia hali yako ya kawaida.

Ni uongjwa ambao utakuweka miezi ukiwa kitandani si wa lolote wala chochote. Kama atakua na mapenzi ya dhati kwako atajali maradhi yako.

Atakosa furaha kipindi chote cha ugonjwa wako. Atapigania kila njia aweze kukufariji na kukupa matumaini hadi hali yako itakaporejea.

Yule aliyekuwa akiigiza tu kipindi cha uzima wako hayo hatoyafanya, atashindwa kwa sababu aliyokuwa akiyafanya hakua akiyafanya kwa dhati.

Mtu wa namna hii atashindwa kukujali na kuona umekuwa mzigo kwake. Kipitia maradhi ni kipimo tosha cha kumjua mwenzawako ni wa namna gani.

KUKOSA WATOTO

Watoto ni zawadi pekee kwa wanandoa kutoka kwa Mungu. Inapotokezea ndani ya ndoa mmoja wapo kukosa kizazi, basi huwa ni kizaa zaa. Maneno ya kashfa, matusi na masimango humuandama mwenye tatizo.

Yapasa tuelewe kuwa, kizazi ni majaaliwa kutoka kwa Mungu na hapangi kiumbe mwenyewe. Hivyo hatuna budi kustahamiliana na sio kutoleana kauli chafu zisizofaa. Hichi ni kipimo chengine cha upendo kwenye ndoa.

Mume au mke mwenye kutambua thamani ya uwepo wa mwenzake, lazima atamjali. Atashirikiana naye kwenye shida na raha. Na pindi litakapotokezea kwa mwenzake tatizo kama hili daima atakua mstari wa mbele kwa kumliwaza na kumfariki.

Hatonyanyua kinywa chake kwa kumsimanga na kumtusi, kwa maana pia anatambua kama hujafa hujaumbika.

Atakuwa naye pamoja kwa kila jambo na kumtaka ushauri jinsi ya kutatua tatizo hilo kama itawezekana. Na kama ikishindikana sio maamuzi ya busara kuachana.

KUPATA MAENDELEO YA GHAFLA

Kama mulikula shida pamoja ya nini mutengane katika raha? Waswahili wana msemo husema, “Unayeokota naye kuni pamoja ndio wa kukoza naye moto”.

Kama alikubali kuolewa na wewe huku akijua hali zenu kimaisha mnalingana, kwa nini sasa baada ya kupata mafanikio anabadilika?

Ana badili sheria kwa kipato tu alichoruzukiwa ambacho kabla hakua nacho. Yeye sasa ndio kawa bwana kwenye nyumba badala ya mume wake.

Amekuwa na sauti kali yenye kuudhi muda wote. Amekuwa na mdomo mchafu wenye maneno ya ajabu ambao kabla hakua nao. Hii ina maanisha mwanamke wa aina hii ameshindwa kwenye kipimo hichi cha upendo kwa wanandoa. Sababu tu ya kiburi chake.

Kipato hakibadili dhamira ya kweli ya mapenzi kwa mwanandoa dhidi ya mwenzake. Kama alimpenda kwa dhati, daima ataendelea kumuheshimu na kumuona ni mume wake kama hapo awali. Kwa kigezo hichi, wanawake wengi wanafeli.

KUTENGANA KWA MUDA

Hapa naomba nieleweke vizuri. Kutengana huku kusiwe kule kuachana. Maana yangu ni kwamba, mfano mzuri mume kusafiri kwa ajili ya kibiashara au kuhamishiwa sehemu ya kazi mbali na nyumbani kwake.

Au kwa wale wanaosafiri na kwenda kufanya kazi nchi nyengine kwa kipindi cha mkataba maalumu. Wengine miaka miwili, wengine mitatu au zaidi huku nyuma wakiacha wake na watoto wao.

Kwa kipimo hichi basi wingi wa wanawake hushindwa na kupoteza sifa za uaminifu kwa wenziwao. Wengi wao huzipitia ndoa zao kwa mlango wa nyuma (Nje ya ndoa), wakisaliti halali na kukimbilia haramu.

Hii husababishwa na tamaa zenye kushambulia kwa kasi hisia za kimwili. Ha tua hii ya kutoka nje ya ndoa pia husababishwa na tabia za awali za uchepuko waliokuwa nao baadhi ya wanawake.

Mwanamke mwenye kujithamini na kujiheshimu hawezi kuyafanya haya ilhali akijijua kuwa yupo kwenye ndoa.

Daima atajitunza na kujihifadhi kwa kuilinda heshima ya mumewe. Hatokubali hata siku moja mtu mwengine kukitumia kitanda cha mumewe akiwa hayupo.

Atakua na yakini kuwa hata mumewe asipomuona wakati akiyatenda hayo, basi Mungu yatosha kumuona. Na yeye ndie wakuogopwa haswaa.

Nakunja jamvi kwa kueka nukta, tukutane wiki ijayo marafiki panapo uhai.