VYAMA vyetu vya siasa viko kwenye mbio za kuwatafuta ama baadhi ya vyama hivyo vimeshawapata wagombea watakaopewa idhini na ridhaa kwa ajili kuwaniwa nafasi mbalimbali za uongozi.

Katika tahariri hii hatutogusia michakato ya kuwapa wagombea wa ngazi za urais, ambapo kwa kawaida kupatikana kwake hufanywa na vikao na kamati za vyama vya siasa za ngazi za juu.

Hata hivyo, tutajikita kujadili japo kwa ufupi kwenye michakato ya vyama vya siasa vya kuwapata wagombea kwenye ngazi za ubunge, uwakilishi na udiwani.

Tunajua unaweza kujiuliza kwanini tujadili viongozi hawa, upo umuhimu kujadili michakato wa vyama vya siasa vilivyowapata wagombea wa ubunge, uwakilishi na udiwani kwa sababu hawa ndio viongozi tunaishi nao kwenye maisha ya kila siku ya miaka mitano ijayo.

Tunaelewa kwenye baadhi ya vyama vya siasa mchakato wa kuwapata viongozi hao umekwisha fanyika katika hatua za awali, na safari inaendelea mbele kwenye vikao vyengine vya ngazi ya juu kwa ajili ya kuridhiwa.

Kabla ya wagombea wa ubunge, uwakilishi na udiwani kuthibitishwa kwenye vikao vya juu, tungependa sana kuwaeleza wakuu wa vikao hivyo wakayaangalia vyema yale yaliyofanyika katika zoezi la kura ya maoni.

Tunaelewa kwenye siasa fitna ni jambo la kawaida, lakini katika baadhi ya maeneo malalamiko yaliyotolewa na yanayoendelea kutolewa na baadhi ya waliogembea kwenye nafasi hizo yana ukweli kwa asilimia kubwa.

Katika hili vikao vikubwa vya vyama vya siasa ni vyema vikachambua ipi fitna ya kushindwa na yepi madai ya kweli ya kuyafanyia kazi, kwa sababu yale yanayoendelea kiukweli hayaridhishi.

Kwa mfano kuna mambo mengi yanayozungumzwa ikiwemo madai ya kuwepo harufu za rushwa na ufisadi, ambapo wale wanaoitwa ‘wajumbe’ wamepokea fedha kwa ajili ya kununuliwa.

Tunajiuliza kama kweli kiongozi anayepitishwa ametoa rushwa je akeshapigiwa kura Oktoba 28 mwaka huu na kuwa mbunge, mwakilishi ama diwani wetu atawezaje kusimamia vita dhidi ya rushwa kama ajenda ya kitaifa?

Wajumbe hawa hadi wameimbiwa nyimbo na kurushwa mitandaoni huku wakielezwa kuwa sio watu, kwa sababu tu baadhi ya waliogombea wanawatuhumu kupokea rushwa ya viwango tofauti vya fedha baina ya jimbo moja na jengine.