NA KHAMISUU ABDALLAH

VITAMBULISHO 566,352 vimezalishwa na Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), kwa ajili ya kuagiwa wapiga kura katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 28 mwaka huu.

Mkurugenzi wa Tume hiyo, Thabit Idarous Faina, alisema kati ya vitambulisho hivyo 272,115 ni vya wanaumme na 294,237 ni vya wanawake.

Alisema kwa wilaya ya Kaskazini ‘A’ vitambulisho vilivyozalishwa vilikuwa 62,117 Kaskazini ‘B’ vitambulisho 40,237, wilaya ya Kati Unguja vitambulisho 51,644 na Kusini Unguja ni vitambulisho 28,985.

Kwa upande wa wilaya ya Magharibi ‘A’ alisema vitambulisho vilivyozalishwa ni 62,701, wilaya ya Magharibi ‘B’ vitambulisho 70,159 na mjini vitambulisho 109,009.

Mkurugenzi Faina alisema kwa Pemba wilaya ya Wete jumla ya vitambulisho 37,195, wilaya ya Micheweni 26,586, wilaya ya Chake Chake 42,933 na wilaya ya Mkoani vitambulisho 34,786.

Aidha alisema katika uzalishaji wa vitambulisho hivyo ZEC imetumia jumla ya shilingi milioni 240 kwa ajili zoezi la ugawaji wa kadi kwa Unguja na Pemba na bilioni 1.2 kwa ajili ya ununuzi wa kadi.

Hata hivyo, alisema kwa wale ambao hawatokuwa na sifa za kupigia kura tume inaendelea kupokea tarifa mbalimbali kwa watu waliofariki hadi pale ZEC itakapofunga daftari la kudumu la wapiga kura siku saba baada ya uteuzi wa wagombea.

Mbali na hayo alisema tume itaendelea kutatua changamoto ya upatikanaji wa vitambulisho kwa wananchi ambao bado hawajenda kuchukua na kuwataka kufika katika ofisi za tume za wilaya iliwaweze kuchukua vitambulisho vyao na kupata haki ya msingi ya kikatiba ya kupiga kura.

“Yoyote ambae amehakiki na anavitu vinavyostaki ikiwemo risiti basi atapatiwa kitambulisho kabla ya siku ya kura katika uchaguzi wa mwaka huu kufanyika,” alisema.

Katika hatua hiyo Tume iIipitia hatua mbalimbali za uchaguzi ikiwemo kuanza rasmi zoezi la uandikishaji wa wapiga kura wapya na uhakiki wa wapiga kura waliokuwemo kwenye daftari la kudumu la wapiga kura Januari 18 mwaka huu, katika wilaya ya Micheweni Pemba na kumalizika rasmi zoezi hilo Machi 4 mwaka huu.

Zoezi hilo kwa mara ya pili lilifanyika katika mikoa yote ya Unguja na Pemba kuanzia Mei 30 hadi Juni 12 mwaka huu uwekaji wazi wa taarifa za wapiga kura ulioanza Julai 8 hadi 14 mwaka huu na ugawaji wa vitambulisho vya kupigia kura wananchi walioandikishwa katika daftari la kudumu la kupigia kura Julai 18 hadi 20 kwa Pemba na Julai 26 hadi 27 kwa kisiwa cha Unguja. 

Hivi karibuni Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) Jaji Mkuu Mstaafu Hamid Mahmoud Hamid, alitangaza tarehe ya uchaguzi Oktoba 28 mwaka huu sambamba na uchaguzi wa Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania.