Ni pori liliwekwa kwenye urithi wa dunia

Na Agnes Benedict

PORI la Akiba la Selous ni kati ya mapori 28 ya akiba chini ya Mamlaka ya Usimamizi Wanyamapori Tanzania (TAWA).

Pori hili lina Ukubwa wa kilomita za mraba 50,000 sawa na asilimia 5 ya ardhi yote ya Tanzania bara ambapo lilianzishwa rasmi mwaka 1896, likijulikana kama“Shamba la Bibi” 1922 lilipewa rasmi jina la Selous.

Kutokana na ukubwa wake pori hili limepakana na mikoa minne ambayo ni Morogoro, Pwani, Ruvuma na Lindi ambapo Wilaya 12 za mikoa hiyo zilizopakana na Pori ni Liwale, Kilwa, Rufiji, Kilombero,Morogoro Vijijini, Ulanga, Namtumbo,Tunduru, Kisarawe, Malinyi, Kilosa na Nachingwea.

Kutokana na umuhimu wake kimataifa pori hili lilitangazwa kuwa eneo la Urithi wa Dunia (World Heritage Site – WHS) mwaka 1982

Aidha, kutokana na kupungua sana kwa idadi ya tembo kwa sababu ya ujangili mwaka 2014, pori la Selous liliingizwa kwenye orodha ya Urithi wa Dunia uliopo hatarini kutoweka.

Meneja wa Pori la Selous, Henock Msocha, anabainisha shughuli kuu zinazofanyika katika pori hilo kuwa ni pamoja na Ulinzi wa rasilimali za wanyamapori na mazingira yao Usimamizi wa Matumizi endelevu ya wanyamapori Udhibiti wa wanyama wakali na waharibifu Ushirikishaji wa jamii katika uhifadhi Shughuli za Maendeleo.

Aidha anasema kutokana na ukubwa wa pori hili, usimamizi wake umegawanywa katika Kanda nane ambazo ni Matambwe, Kingupira, Miguruwe, Liwale, Kalulu Likuyu, Sekamaganga, Msolwa na Ilonga.

Akizungumzia kuhusiana na ulinzi, anasema kwa kawaida hufanyika kwa kufanya doria ndefu na fupi ndani na nje ya pori ili kuhakikisha rasilimali zilizopo zinalindwa ipasavyo.

“Tunavishirikisha vikundi vya doria vyenye wastani wa askari sita kufanya doria kwa siku 15 kila mwezi”, alisema.

“Menejimenti ya Pori la Akiba Selous inaendelea kuimarisha miundombinu pamoja na kuhakikishaupatikanaji wa vitendea kazi vya kutosha ili kuongeza ufanisi katika doria hizo”.

Akizungumzia kuhusu usimamizi wa matumizi endelevu ya wanyamapori, alisema kuwa Shughuli za matumizi ya wanyamapori zinazofanyika katika pori la akiba Selous ni utalii wa picha na uwindaji wa kitalii ambapo hufanyika katika vitalu  vya Matambwe na Uwindaji wa kitalii katika vitalu vya kanda nyingine.

Akifafanua zaidi anasema kuwa zipo kambi za kitalii 11 zilizojengwa ndani ya pori la akiba Selous na 14 zimejengwa maeneo ya vijiji kwa ajili ya utalii wa picha.

Alisema katika kipindi cha mwaka wa fedha 2017/18 doria zenye jumla ya watu 92,587 zilifanyika ambapo kiasi cha shilingi 3,893,549,749 zilitumika kugharamia doria hizo Jumla ya watuhumiwa 786 wa makosa mbalimbali ya ujangili walikamatwa.

Sambamba na hilo, lakini meneja huyo anasema kuwa nyaya za kutegea wanyamapori (rada) 491 na bunduki 84 na risasi 345 vilikamatwa huku nyamapori zenye uzito wa kilogramu 4,360.9 zilikamatwa.

“Hii inadhihirishwa na kupungua kwa vifo vya tembo vilivyotokana na ujangili ambapo menejimenti ya pori la akiba Selous inaendelea kuimarisha miundombinu pamoja na kuhakikisha upatikanaji wa vitendea kazi vya kutosha ilikuongeza ufanisi katika doria hizo”, alisema.

Aidha alisema Utalii wa picha hufanyika katika vitalu vitano vya Matambwe na Uwindaji wa kitalii katika vitalu vya kanda nyingine zipo kambi za kitalii 11 zilizojengwa ndani ya pori la Akiba Selous na 14 zimejengwa maeneo ya vijiji kwa ajili ya utalii wa picha.

Anaongeza kuwa pori la akiba Selous hupokea wastani wa watalii 22,000 (wasio wazawa) na 8,000 wazawa kwa kila msimu.

“Watalii hao hufanya game drive, safari za matembezi, michezo ya kuogelea nakadhalika ambavyo vyote kwa ujumla wake ni vivutio vikubwa vilivyopo na kwamba kuna wanyamapori wa aina mbalimbali, mandhari nzuri ya uoto wa asili, mandhari ya mto Rufiji na Ruaha na maziwa, kaburi la Selous, chemchem ya maji moto ni vitu vinavyopatikana”, alisema.

Meneja huyo anasema kuwa katika mwaka 2017/18 jumla ya watalii 26,454 walitembelea pori la Selous ambapo takwimu zinaonesha kuwa idadi ya watalii imeongezeka ikilinganishwa na watalii 23,490 waliotembelea mwaka 2016/17

Jumla ya Shilingi za kitanzania 436,099,784.76 na dola za kimarekani 2,722,899.90 zilikusanywa huku vitalu 42 vya kanda saba zilizobaki vimetegwa kwa ajili ya uwindaji wa kitalii shughuli za uwindaji wa kitalii hufanyika kuanzia mwezi Julai hadi Disemba kila mwaka.

Anafafanua kuwa hifadhi ya utalii alisema kuwa katika kipindi cha msimu wa uwindaji cha mwaka wa fedha 2017/18 kampuni 18 zilifanya shughuli za uwindaji

Alizataka kampuni hizo zilizotumika kwa uwindaji katika vitalu 34 ziliingiza wageni wawindaji 151 wakiandamana na watazamaji (observers) 127 waliwinda wanyama tofauti katika vitalu hivyo.

Kwa mujibu wa meneja huyo, takwimu zinaonesha kuwa idadi ya wageni wanaotembelea Selous kwa ajili ya uwindaji wakitalii imekuwa ikipungua mwaka hadi mwaka hio inatokana na  uwindaji wa kitalii kupunguza mapato yatokanayo na shughuli hizo.

Alizitaja sababu za kushuka kwa idadi ya wageni hao, alisema zinatokana na baadhi ya nchi hususan Marekani na baadhi ya nchi za jumuiya ya Ulaya kuzuia uingizaji wa nyara za tembo na simba katika nchi zao.

Hata hivyo, meneja huyo anasema kuwa pamoja na faida iliyopo katika pori hilo la akiba lakini kumekuwa na changamoto kadhaa zinazowapata wanavijiji ikiwa ni pamoja na wanyama wakali kuingia vijijini.

“Wanyama wanaoingia katika maeneo ya vijiji ni pamoja na tembo, nyani, fisi, simba, chui, nyati na viboko ambao ni hatari kwa wanaadamu”, alisema.

“Kanda za Kalulu, Kingupira, Msolwa na Seka huwa na matukio mengi ya wanyama waharibifu kuliko kanda nyingine katika kipindi cha mwaka wa fedha 2017/18 doria zilidhibiti wanyama wakali na waharibifu ambapo siku 1,537 zilifanyika doria hizo na kwamba jumla ya watu sita waliuwawa na tisa  walijeruhiwa kwa kushambuliwa na wanyamapori wakali”, alisema.

Aliongeza kuwa jumla ya hekari 163 za mazao mbalimbali ya wananchi ziliharibiwa na wanyamapori katika juhudi za kulinda mali na maisha, huku wanyamapori wanane wakiwemo (viboko sita, mamba mmoja na fisi mmoja) waliovamia katika maeneo ya vijiji waliuwawa kwa kupigwa risasi na askari.

Menejimenti ya pori pia inashiriki katika kutoa huduma za kijamii mfano wa ujenzi wa madarasa, zahanati, barabara, upatikanaji wa maji safi.

Vipaumbele vyengine ni pamoja na kutoa ajira katika kambi za utalii ambapo baadhi ya watumishi wamepata mafunzo ya intelijensia, uendeshaji wa kesi mahakamani, ufundi wa magari na udereva, ufanyaji wa demografia ya tembo.

Uboreshaji wa mawasiliano ndani ya pori, uboreshaji wa vitendea kazi vya doria kama magari, GPS, mahema, ufanyaji wa sensa ya wanyamapori wakubwa ndani ya Ikolojia ya Selous ni mambo yanayopewa vipaumbele.

Hata hivyo, meneja huyo anasema kuwa pori la akiba Selous linakabiliwa na changamoto ya ujangili hasa wa nyama pori ambapo alisema ongezeko la mifugo kandokando mwa pori hasa katika kanda za Matambwe, Kingupira na Ilonga

Uchache wa nyumba kwa ajili ya makaazi ya watumishi ambapo karibu asilimia 50 ya watumishi hawana mahala pa kuishi ni mambo mengine ambayo yanakusudiwa kuimarishwa katika pori hilo muhimu kwa hifadhi ya taifa.

Kwa mantiki hiyo basi, pori Selous ni muhimu sana kwa kuwa ni moja linaloingiza mapato ya serikali.