Azindua, aweka mawe ya msingi miradi ya ujenzi

NA RAJAB MKASABA, IKULU

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein amesema kuwa serikali imechaguliwa na wananchi ni kuwapatia huduma kwani wao ndio waliyoiweka madarakani.

Dk. Shein alieleza hayo katika uwanja wa Zimamoto bandarini, Mkoani Pemba wakati akizungumza na wananchi mara baada ya kuweka jiwe la msingi la ofisi za ZSSF Tibirinzi, ofisi za ZRB Gombani na kuzindua hoteli ya Mkoani ambayo imefanyiwa ukarabati.

Alisema kazi  ya serikali ni kuwaletea maendeleo wananchi na kwamba serikali ya awamu ya saba imekuwa ikifanya hivyo kwa vitendo jukumu la  kuwasogezea huduma muhimu za kimaisha.

Alifahamisha kuwa baada ya mapinduzi ya mwaka 1964, serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imetekeleza ahadi zilizoahidiwa na Chama cha ASP.

Alieleza hivi sasa serikali inatekeleza ahadi za Chama cha Mapinduzi  ilizoahidi katika ilani ya uchaguzi ya mwaka 2015-2020, ikiwa ni kuwahudumia wananchi.

Dk. Shein alisema kuzinduliwa kwa hoteli ya Mkoani  ambayo ni miongoni mwa hoteli za serikali sambamba na ya ChakeChake na ya Wete ambazo zilikuwa chini ya shirika la Utalii ambalo kwa sasa halipo, ilikuwa ni kuwahudumia wananchi wa ndani na nje ya nchi.

Alisema kuwa hoteli ni kwa ajili ya watu mbali mbali wakiwemo watalii na wananchi ambao wanapata huduma za kitalii ambayo hatua hiyo inaimarisha utalii wa ndani.

Dk. Shein aliwanasihi wananchi kwa upande wao kujenga hoteli kwani tayari ZSSF imeonesha njia na serikali imewaamini huku akisisitiza makampuni, mashirika na wajasiriamali nao kufanya hivyo.

Alieleza kuwa serikali zilizopita za kikoloni hazikuimarisha sekta ya kitalii na badala yake serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeimarisha kwa kiasi kikubwa sekta hiyo tokea Mapinduzi na kusababisha kuongezeka kwa hoteli na wageni.

Kwa upande wa hatua za serikali za kujenga jengo la ZRB, Dk. Shein alisema kuwa hatua hiyo itasaidia kwa kiasi kikubwa kukusanya kodi kwa ajili ya mapato ya Zanzibar.

Aliongeza kuwa ZRB imefanya kazi kubwa na ndio maana uchumi wa Zanzibar umeimarika na hivi sasa kufikia uchumi wa kati kama ilivyo kwa upande wa Tanzania bara ambapo hivi sasa uchumi wa Zanzibar umekua kwa asilimia saba.

Alisema kuwa hivi sasa serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imekuwa ikifanya mambo yake wenyewe kwa kutegemea fedha zake inazozikusanya.

Kwa upande wa ofisi za ZSSF zinazojengwa huko Tibirinzi, Dk. Shein alisema kuwa kujengwa kwa ofisi kutasaidia kwa kiasi kikubwa kuwawekea mazingira mazuri wafanyakazi.

Dk. Shein alisema kuwa ZSSF imeanzisha miradi mikubwa Unguja na Pemba hatua ambayo imesababisha kukua na kuimarika kwa miji yote ya Zanzibar.

Awali Dk. Shein alipokuwa akiweka mawe ya msingi katika ofisi za ZSSF huko Tibirinzi na ZRB huko Gombani alisema miradi kadhaa inatarajiwa kuendelezwa na mingine kuanzwa ukiwemo ujenzi wa uwanja wa ndege wa Pemba.

Katika mkutano huo huko Mkoani, waziri wa Fedha na Mipango Balozi Mohammed Ramia Abdiwawa alieleza mafanikio yaliyopatikana kutoka mfuko wa ZSSF na kutoa historia ya ujenzi wa hoteli kisiwani humo.

Balozi Ramia aliwaondoa wasiwasi wananchi na kuwaeleza kwamba fedha zao zilizoko katika Mfuko wa Jamii wa ZSSF ziko salama.

Naye Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango Khamis Mussa alisema kuwa maendeleo yameendelea kupatikana hapa nchini katika miaka 10 ikiwemo katika uwekezaji wa ofisi za serikali na taasisi zake.

Alisema kuwa kwa upande wa hoteli ya Mkoani, hoteli hiyo ilifunguliwa Januari 9, 1974 na kutoa huduma kwa miaka 1970 hadi 1990 ambapo kutokana na kukosa matunzo yanayopaswa hoteli ilichakaa na kusita huduma zake.

Alieleza kuwa chini ya uongozi wa Dk. Shein, Baraza la Mapinduzi liliamua kuikabidhi hoteli hiyo kwa ZSSF kwa lengo la kuifufua na kuiendeleza kiuchumi kama lengo la awali la kuijenga kwake ambapo makabidhiano rasmi yalifanyika Oktoba 19 mwaka 2018.