NA NASRA MANZI

MUFTI Mkuu wa  Zanzibar Saleh Omar  Kaabi amewashauri  viongozi watakao chaguliwa  kuiongoza  Zanzibar, kuendeleza amani ya nchi, sambamba   na kufuata  nyayo za Rais  wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk.  Ali Mohamed Shein kwa kuleta maendeleo katika nyanja tofauti.

Kauli hiyo ameitoa baada ya Waziri wa Nchi kufanya  ziara fupi katika Ofisi zake zilizopo Mazizini, alisema endapo viongozi hao wataongoza kwa uaminifu na uadilifu mapungufu yaliyokuwepo kuyaondosha na kuifanya nchi kuendelea na utulivu iliyotawaliwa na busara.

Pia alisema Zanzibar imejaliwa kuwa na amani na wananchi wamekuwa wakifanya shughuli zao za kujiletea mafanikio, hivyo haitakuwa busara kwa wale watakaoharibu amani kuachiliwa ni vyema kuchukuliwa hatua kwa mujibu wa Sheria.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Haroun Ali Suleiman, alisema wananchi hawanabudi kudumisha amani iliyokuepo katika kipindi hichi cha kuelekea uchaguzi mkuu na kujiepusha kujiingiza katika vikundi vitakavyoashiria vurugu.

Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Said Hassan Said, alisema mashirikiano yanahitajika katika kuiombea nchi, ili kufanya uchaguzi kuwa wa salama na amani.