NA HAJI NASSOR, PEMBA

MASHTAKIWA Salum Massoud Bakari wa Ukutini Wilaya ya Mkoani, ambae anadaiwa kuiba friji yeye na mwenzake, ameiambia mahakama ya Mkoa Chake Chake kuwa, Polisi wa Kituo cha Mtambile walimlazimisha kusema kuwa ameiba , ingawa hahusiki na wizi huo.

Akiwa kwenye kizimba cha mahakama hiyo, wakati akitoa maelezo yake ya utetezi, alidai kuwa hata afya ya akili haikuwa vyema sana, baada ya kupokea kichapo kutoka kwa askari hao.

Alidai kuwa, hahusika na kuvunja duka na kisha kuiba friji hilo yeye na mwenzake, ingawa maelezo ya Polisi yalionesha ametenda kosa hilo.

“Ni kweli wakati nachukuliwa maelezo pale kituo cha Polisi Mtambile sikuwa hadhari sana, maana kwanza walishanipiga vizuri Polisi, kisha wakanilazimisha nikiri kosa, lakini mimi sihusiki,’’alidai mshtakiwa huyo.

Aidha mshitakiwa huyo alidai kuwa, Polisi walipaswa kufuata sheria na kanuni zinavyoelekeza, na sio kuchukua hatua za kumpiga na kisha kumlazimisha kusema jambo ambalo halielewi.

Nae Mshitakiwa namba mbili kwenye shauri hilo, Hadhara Abdi Abass, aliimbia mahakama hiyo, hahusiki na wizi huo na wala hakumbuki kufanya jambo la aina hiyo.

Alidaiwa kuwa, amekuwa na shughuli zake za kila siku za uendeshaji wa boda boda, ili kujitafutia riziki, na hajawahi kuvunja duka na kuiba, kama ilivyoelezwa mahakamani hapo.