NA HANIFA SALIM, PEMBA

MWENYEKITI wa chama cha Allance for Democratic Change (ADC) Hamadi Rashid Mohamed amesema, chama chake kitaendesha kampeni za kistaarabu huku kikiheshimu mawazo ya vyama vyengine ili kuepusha migongano kwa jamii.

Alisema, chama chake hakitakuwa miongoni mwa vyama ambavyo vitachangia au kuwashawishi wananchama wake kusababisha migogoro ya aina yoyote kwa wanachama baada au kabala ya uchaguzi.

Aliyasema hayo, wakati akizungumza na wafuasi wa chama cha ADC mara baada ya kuzindua tawi jipya la chama hicho huko Mkanyageni Wilaya ya Mkoani Mkoa wa Kusuni Pemba.

Hamad alieleza kuwa, kuna maisha baada ya uchaguzi hivyo aliwataka wanachama wa chama hicho kuwa watulivu katika kipindi chote cha uchaguzi kwa kuendelea kuilinda amani na utulivu iliyopo nchini.

“Wanachama nawaombeni kujitokeza kuchukuwa fomu za kugombea nafasi za uongozi ndani ADC ili tuweze kusimamisha wagombea katika majimbo mbali mbali ikiwa ni njia moja wapo ya kukipatia ushindi chama chetu” alisema.

Aidha, aliwataka vijana kuacha kulalamikia suala la ukosefu wa ajira kwani alisema, ADC endapo itapata ushindi na kuongoza nchi tatizo hilo itapata njia kumaliza, kwani chama hicho kina mipango bora kwa Zanzibar pindi itakapo ingia madarakani.

Mapema, Mkurungezi wa Mipango na Uchaguzi wa chama hicho Pemba Omar Kostatin, aliwataka wanachama hao kuwa wazalendo, kujituma, kuitumikia nchi yao, huku wakiwa na mashirikiano ya pamoja katika uchaguzi mkuu.