NA TATU MAKAME

MUSTAFA Mawazo Mustafa (32) mkaazi wa Kitundu Wilaya ya Magharibi ‘A’ Unguja, amefariki dunia baada ya kunaswa na umeme.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja, Awadhi Juma Haji, akizungumza na waandishi wa habari Ofisini kwake Madema Wilaya ya Mjini alisema tukio hilo lilitokea mwishoni mwa wiki iliyopita.

Alifahamisha kuwa marehemu kabla ya kifo chake, alikuwa katika shughuli zake za kuunganisha waya kienyeji kwenye nyumba na ndipo ilipotokezea shoti na kumrusha na kumsababishia kifo.

Hata hivyo, Kamanda Awadhi, alisema mwili wa marehemu ulifanyiwa uchunguzi Hospitali ya Mnazimmoja kisha kukabidhiwa jamaa zake kwa ajili ya mazishi na  aliwataka wananchi kuwa makini wakati wanapotumia vifaa vya umeme ili kujiepusha na madhara.

Aidha, aliwataka wananchi wanaotaka kuungiwa huduma hiyo kufuata sheria kwa kwenda kwa Shirika la umeme, ili kupatiwa mafundi watakaofanya kazi kwa umakini na kuacha kutafuta fundi watakaounga huduma hiyo kwa kutofuata sheria ili kujiepusha na majanga.