KABUL,AFGHANISTAN

SERIKALI  ya Afghanistan imesema  kuwa haitowaachia huru wafungwa 320 waliobaki wa kundi la wanamgambo la Taliban, hadi pale kundi hilo litakapowaachia maofisa wa Serikali.

Tangazo hilo kwa mara nyengine linayaweka rehani mazungumzo ya amani yaliyokuwa yamepangwa kuanza ndani ya siku chache zijazo.

Ufaransa na Australia zinaunga mkono uamuzi wa Serikali ya Afghanistan.

Wiki iliyopita baraza la taifa la kijadi lilifikia makubaliano ya kuwaachia wafungwa 400.

Baadhi yao wamo wafungwa waliofanya mashambulizi dhidi ya maofisa wa Serikali na Raia wa kigeni.

Tangu wakati huo ni wafungwa 80 tu walioachiliwa kabla ya Serikali kusimamisha zoezi hilo.

Wafungwa hao 400 wangekuwa wa mwisho kati ya wafungwa 5,000 wa kundi la Taliban wanaotakiwa kuachiwa na Serikali kwa mabadilishano ya maofisa 1,000 wa Serikali kutoka mikononi mwa wanamgambo.