NAIROBI,KENYA

KITUO  cha Kinga na Udhibiti wa Magonjwa cha Afrika, Africa CDC kimezitaka Serikali za Afrika kuongeza kasi ya ufuatiliaji, upimaji, utafutaji wa watu waliokuwa karibu na wenye virusi vya Corona na kuwahudumia wagonjwa wa COVID-19, kufuatia kusambaa kwa kasi kwa virusi hivyo barani humo.

Kituo hicho kilitoa wito huo wa dharura kwenye ripoti yake mpya ya Afya ya Umma na Utekelezaji wa hatua za jamii katika Afrika ambayo ilichambua mienendo mikuu inayoendelea kwenye janga la COVID-19 barani Afrika katika wiki iliyopita.

Kulingana na ripoti, idadi ya maambukizi mapya ya COVID-19 yaliyoripotiwa yamepungua kwa asilimia 23 katika wiki iliyopita yakilinganishwa na wiki ya nyuma yake, huku vifo vipya vikiongezeka kwa asilimia kumi katika wakati kama huo.