Afrika itatangazwa kuumaliza ugonjwa wa polio na Tume ya Ukanda wa Afrika ya kupambana na Polio kwa kawaida ugonjwa huo huathiri watoto walio chini ya umri wa miaka mitano, wakati mwingine husababisha kupooza.

Ugonjwa wa polio husababishwa na kirusi ambacho husambaa kutoka kwa mtu mmoja kwenda kwa mwingine kupitia maji yaliyochafuka, ambapo kirusi hicho kinaweza kusababisha kupooza kwa kushambulia mfumo wa fahamu.

Kwa mujibu wa wataalamu wa afya, polio pia inaweza kusababisha kifo iwapo kupooza huko kutaathiri misuli inayosaidia mfumo wa upumuaji kwa mgonjwa waliyeambukizwa ugonjwa huo.

Kwa hakika hakuna tiba ya kutibu ugonjwa huo, lakini wataalam wamepiga hatua kubwa kuumaliza ugonjwa huo katika maeneo mbalimbali duniani kupitia chanjo ambayo huwalinda watoto na kutokuwepo uwezekano wa  kupata ugonjwa huo katika maisha yao yote.

Kwa mujibu wa tafiti za tiba, ugonjwa huo umetokomezwa maeneo mbalimbali ikiwemo Afrika, lakini tafiti hizo zimebainisha kuwa bado nchi kama Afghanistan na Pakistan bado umekuwa ukisumbua.

Barani Afrika, Nigeria ni nchi ya mwisho kutangazwa kuutokomeza ugonjwa huo mbaya, ambayo ilikuwa na wagonjwa zaidi ya nusu ya wagonjwa wote wa polio duniani katika kipindi cha miaka 10 iliyopita.

Takwimu zinaonesha kuwa aina mbili kati ya tatu ya virusi vya polio vimeondolewa duniani, ambapo barani Afrika muda sio mrefu kutoka sasa ugonjwa huo utatangazwa rasmi kuwa umeweza kukabiliwa.

Zaidi ya watoto asilimia 95 ya watu wote barani Afrika wamepatiwa kinga ya ugonjwa, hali hiyo ilikuwa moja ya masharti yaliyowekwa na kamisheni kabla ya kulitangaza bara la Afrika kuwa limedhibiti rasmi ugonjwa huo.

Shirika la Afya duniani (WHO), limebainisha kuwepo kwa wagonjwa wachache sana katika baadhi ya nchi za Afrika ikiwemo Nigeria, Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Jamuhuri ya Afrika ya Kati na Angola.

Afrika imewezaje kutokomeza vipi polio? Bila dawa, chanjo ilitengenezwa mwaka 1952 na Dk. Jonas Salk ilitoa matumaini kuwa watoto wanaweza kulindwa dhidi ya ugonjwa wa polio kwa kutumia chanjo.

Mnamo mwaka 1961 polio iliwaathiri zaidi ya watoto 75,000 barani Afrika, ambapo kila nchi iliathirika na ugonjwa huo.

Aidha mnamo mwaka 1996 aliyekuwa rais wa Afrika Kusini, hayati Nelson Mandela alianzisha programu ya ”Ondoa Polio Afrika”, akiwahamasisha wafanyakazi wa afya ambao walikwenda hadi vijijini kutoa chanjo ya kukinga ugonjwa huo.

Tangu mwaka 1996 chanjo za matone bilioni tisa zimetolewa sehemu mbalimbali duniani na kusababisha watoto ambao ndio waathirika wakubwa wa ugonjwa huo kukingwa na kutopata ugonjwa huo.

Bila shaka kwenye suala zima la kinga dhidi ya polio, changamoto kadhaa zilikuwepo hasa barani Afrika ikiwemo tatizo la jamii zilizokuwa hatarini kuathiriwa na polio kuishi katika baadhi ya maeneo yaliyo magumu kufikiwa na kampeni ya chanjo.

Nigeria ni nchi ya mwisho Afrika kuripoti kuwa na ugonjwa wa polio, katika jimbo la Borno Kaskazini maeneo ya mbali ya kaskazini mwamashariki na kitovu cha wanamgambo ya Boko Haram yalivamia mwaka 2016, yalikuwa vigumu fikiwa kuwapa watoto chanjo ya ugonjwa huo.

Mzozo na machafuko yanayosababishwa na wanamgambo wa Boko Haram umefanya kuwa vigumu kwa sehemu kadhaa za Nigeria kufikiwa, hasa katika jimbo Borno.

Mbali na Nigeria, sehemu ya mwisho kushuhudia wagonjwa wa polio ilikuwa eneo la mji wa Puntland liliopo Somalia mwaka 2014.

Wafanyakazi wa mstari wa mbele, asilimia 95 miongoni mwao wanawake, walisafiri kuelekea kwenye maeneo yenye mizozo kama vile kupitia Ziwa Chad kwa boti na kuwapatia chanjo jamii ziishizo maeneo ya mbali.

Kampeni ya kukabiliana na polio pia ilikabiliwa na tetesi zilizosambaa na taarifa za kupotosha kuhusu chanjo hiyo ambapo hali hiyo imerudisha nyuma jitihada za chanjo.

Kwa mfano mnamo mwaka 2003 mji wa Kano na maeneo mengine kadhaa ya majimbo ya kaskazini ya Nigeria yalisitisha utoaji wa chanjo hiyo kwa watoto kutokana na ya kuwepo ripoti za viongozi wa dini ya kiislamu kuwa chanjo ilikuwa na dawa ya kuzuia jamii za kiislamu zisiwe na kizazi.

Vipomo vya maabara vilivyofanywa na wanasayansi wa Nigeria, havikukubaliana na shutuma hizo na kwamba kampeni ya chanjo ya polio iliendelea kutolewa.

Mwaka 2013 watoa chanjo wanawake tisa waliuawa baada ya kufyatuliwa risasi na watu waliodhaniwa kuwa ni wapiganaji wa kundi lenye kuendesha harakati za kigaidi la Boko Haram.

Wanawake hao walifyatuliwa risasi wakitekeleza majukumu yao ya kupwatia chanjo watoto ili waepukane na ugonjwa huo kabla ya kuvamiwa na wapiganaji wa Boko Haram.

Ilichukua miongo kadhaa kufanikiwa kuondokana na taarifa za kupotosha kuhusu chanjo, polio inaweza kuingia kwenye nchi isiyo na ugonjwa huo na kusambaa haraka sana na kuathiri watu ambao hawana kinga.

Hii ilitokea Angola, ambayo pamoja na vita vya wenyewe kwa wenyewe, waliweza kudhibiti ugonjwa huo mnamo mwaka 2001.

Nchi hiyo iliendelea katika hali hiyo kwa miaka minne mpaka mwaka 2005 ambapo kuliibuka ugonjwa huo tena ikiaminika kuwa maambukizi yalitoka nje ya nchi.

WHO imesema kuwa ni muhimu kwa nchi kubaki katika hali ya tahadhari mpaka pale ulimwengu utakapokuwa umeutokomeza ugonjwa huo kabisa.