NA KHAMISUU ABDALLAH
BEJI ya udereva imemsababishia Yussuf Rashid Othman (47) mkaazi wa Magombeni wilaya ya Mjini Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja, kufikishwa mahakamani kwa tuhuma za makosa ya barabarani.
Mshitakiwa huyo ambae alikuwa ni dereva wa gari yenye namba za usajili Z 914 CZ iendayo njia namba 339 alifikishwa mahakamani hapo mbele ya Hakimu Amina Mohammed Makame, na kusomewa mashitaka yanayomkabili na Mwendesha Mashitaka wa Koplo wa Polisi Salum Ali.
Ilidaiwa kuwa mshitakiwa huyo akiwa dereva wa gari hiyo akitokea Benbella kuelekea Mnazimmoja alipatikana akiwa hakuvaa beji ya udereva kitendo ambacho ni kosa kisheria.
Tukio hilo alidaiwa kulitenda Julai 22, mwaka huu, majira ya saa 3:45 asubuhi huko Mnazimmoja Wilaya ya Mjini Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja.
Mshitakiwa huyo aliposomewa shitaka hilo alilikubali na kuiomba mahakama imsamehe kwa madai kuwa ndio kosa lake la mwanzo huku upande wa mashitaka ukidai kuwa hauna kumbukumbu ya makosa ya nyuma kwa mshitakiwa huyo, hivyo adhabu itolewe kwa mujibu wa shitaka alilopatikana nalo.
Hakimu Amina, alimtia hatiani mshitakiwa huyo na kumuona ni mkosa kisheria na kumpa adhabu ya kulipa faini ya shilingi 10,000 na akishindwa aende jela wiki mbili.
Mshitakiwa huyo alikamilisha faini hiyo ili kujinusuru kwenda Chuo cha Mafunzo kwa muda wa wiki mbili.