NA KHAMISUU ABDALLAH
KETE 19 zinazodaiwa kuwa ni majani makavu yanayoaminiwa kuwa ni dawa za kulevya aina ya bangi, zimemsababishia kijana mwenye umri wa miaka 23 kufikishwa mahakamani.
Mshitakiwa huyo ni Ibrahim Silima Juma mkaazi wa Mkele wilaya ya Mjini Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja.
Kwa mujibu wa hati ya mashitaka iliyowasilishwa katika mahakama ya Hakimu Mdhamini wa mahakama hiyo, Mohammed Subeit na kusomwa na Mwendesha Mashitaka, Wakili wa serikali kutoka Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP), Mohammed Haji Kombo, ilidaiwa kuwa mshitakiwa huyo alipatikana na kosa la kupatikana na kiwango kidogo cha dawa za kulevya.
Ilidaiwa mahakamani hapo kuwa, bila ya halali alipatikana na furushi moja la gazeti ndani yake mkiwa na kete 19 za majani makavu, ambayo ni dawa za kulevya aina ya bangi yenye uzito wa 13.224 gramu yakiwa yamehifadhiwa ndani ya karatasi ya kaki, kitendo ambacho ni kosa kisheria.