NA MARYAM HASSAN
MARA baada ya upande wa mashitaka kuwasilisha mahakamani mashahidi watatu dhidi ya kesi ya kutorosha na kulawiti mtoto wa kiume wa miaka 17, hatimae mshitakiwa wa kesi hiyo amedai anaumwa na hawezi kuwasikiliza.
Mshitakiwa huyo ni Hassan Khamis Saaduni (40) mkaazi wa Mtoni Toronto, ambaye alitoa madai hayo mbele ya Hakimu Hussein Makame wa mahakama ya mkoa Vuga, wakati kesi hiyo ilipofikishwa kwa ajili ya kusikilizwa.
Mshitakiwa huyo bila ya kuitajia mahakama kile kinachomsumbua, lakini alidai hayupo vizuri hali yake ya afya kwa madai anaumwa na hatoweza kuwasikiliza mashahidi hao.
Mapema kesi hiyo ikiwa mahakamani hapo, upande wa mashitaka chini ya Wakili wa serikali Issa Salim, kutoka Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP), ulidaiwa umepokea mashahidi watatu kwa ajili ya kusikilizwa.
Mara baada ya maelezo hayo ya upande wa mashitaka, mshitakiwa huyo aliiambia mahakama kwa kudai hayupo hali nzuri kiafya kwa maana anaumwa, hivyo hayuko tayari kuwasikiliza mashahidi hao.
Baada ya hoja hizo za mshitakiwa, pande wa mashitaka nao kwa upande wake ulidai kuwa, licha ya kuwasilisha mashahidi hao lakini nao pia umedharurika hivyo hautaweza kuwasikiliza mashahidi hao.
Hivyo badala yake umeiomba mahakama kuiahirisha kesi hiyo na kuipangia tarehe nyengine kwa ajili ya kusikilizwa.
Sambamba na hilo, upande huo wa mashitaka pia umeiomba mahakama kuwaonya mashahidi hao na kuwataka kufika mahakamani hapo tarehe watakayopangiwa ili kutoa ushahidi wao.
Hakimu Hussein, alikubaliana na hoja za pande zote mbili, huku akiiahirisha kesi hiyo hadi Agosti 18 mwaka huu kwa ajili ya kusikilizwa pamoja na kuwaonya mashahidi hao na kufika siku hiyo.
Katika kesi hiyo, Hassan Khamis Saaduni, ameshitakiwa kwa kosa la kumtorosha mtoto wa kiume mwenye umri wa miaka 17 ambaye yupo chini ya uangalizi wa wazazi wake, tukio ambalo alidaiwa kulitenda Machi 18 mwaka huu majira ya saa 2:00 za usiku huko Mwembe Kisonge wilaya ya Mjini Unguja.
Pamoja na tukio hilo la utoroshaji, mshitakiwa huyo anatuhumiwa kumwingilia kinyume cha maumbile mtoto huyo, kitendo ambacho ni kinyume na kifungu cha 116 cha sheria namba 6 ya mwaka 2018 sheria za Zanzibar.
Kosa hilo anadaiwa kutenda Machi 18 mwaka huu majira ya saa 2:00 za usiku hadi Machi 19 majira ya saa 12:00 za asubuhi, jambo ambalo ni kosa kisheria.
Mshitakiwa huyo amepelekwa rumande hadi Agosti 18 mwaka huu, kesi yake itakapoanza kusikilizwa ushahidi.