NA MARYAM HASSAN
MAHAKAMA kuu Vuga, chini ya Jaji Rabia Hussein Mohammed, imemuachia huru mshitakiwa Haji Malik Suleiman (33) mkaazi wa Kwarara, aliyeshitakiwa kwa kosa la mauaji.
Jaji Rabia amemuachia huru mshitakiwa huyo kwa sababu ya kubaini tofauti, mahali kilipokuwepo kisu ambacho anadaiwa mshitakiwa kukitumia wakati wa tukio.
Alisema katika maelezo ya shahidi namba tisa Said Juma, alisema alikuta kisu kikiwa kimeroa damu maeneo ya Mpendae, wakati tukio limetokea Migombani Kaburi kikombe.
Alisema maelezo hayo ndio yaliyomfanya kumuachilia huru mshitakiwa, huku upande wa mashitaka nao ukionekana kushindwa kuthibitisha kosa hilo.
Mshitakiwa huyo alifikishwa mahakamani hapo kwa kosa la kuua kwa makusudi, tukio ambalo linadaiwa kutokea Agosti 5 mwaka 2014 majira ya saa 7:45 za mchana.
Ilidaiwa kuwa, alimuua Said Mohammed Hamadi kwa kumchoma kisu jambo ambalo limepelekea kifo chake.
Kesi hiyo imeanza kusikilizwa ushahidi Julai 1 mwaka 2015 na jumla ya mashahidi tisa walisikilizwa, lakini ushahidi huo haukukidhi mahakamani hapo.
Wakati maamuzi hayo yanatolewa, upande wa mashitaka ulikuwa ukiongozwa na wakili wa serikali kutoka Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP), Othman Senga.
Aidha kwa upande wa mshitakiwa alikuwa akiongozwa na wakili wa kujitegemea Mussa Shaali.