NA KHAMISUU ABDALLAH
BAADA ya Makama ya mwanzo Mwanakwerekwe kutaka kusikiliza ushahidi wa kesi inayomkabili mshitakiwa Salum Ali Malik (26) mkaazi wa Makunduchi Mkoa wa Kusini Unguja, ambae anakabiliwa na shitaka la kuwachoma watoto sita sindano hatimae akubali makosa yake.
Hakimu Mohammed Ali Kombo, wa mahakama hiyo alimtia hatiani mshitakiwa huyo na kumtaka kulipa faini ya shilingi 50,000 kwa kila kosa na kulipa fidia ya shilingi 100,000 kwa kila muathirika na akishindwa atatumikia Chuo cha Mafunzo kwa muda wa mwezi mmoja kwa kila kosa.
Mwendesha Mashitaka Koplo wa Polisi Vuai Ali Vuai, alidai kuwa mshitakiwa huyo alipatikana na makosa sita ya shambulio la kawaida kinyume na kifungu cha 229 cha sheria ya makosa ya jinai namba 6 ya mwaka 2018 sheria za Zanzibar.
Ilidaiwa kuwa, mshitakiwa huyo Januari 10 mwaka huu, saa 10:00 jioni huko Kwamtipura wilaya ya Mjini Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja, bila ya halali alimshambulia Hafidh Rashid Omar, mwenye umri wa miaka minne kwa kumchoma sindano katika kidole cha mkono wake wa kulia na kumsababishia kupata maumuvu makali mwili mwake.
Aidha hati hiyo pia ilidai kuwa mshitakiwa huyo siku hiyo hiyo katika maeneo hayo, alimshambulia mtoto Mudrik Muridu Azani mwenye umri wa miaka mitano kitendo ambacho ni kosa kisheria.
Katika kosa jengine mshitakiwa huyo alidaiwa kumchoma sindano katika kiwiko cha mkono wake wa kulia Abdullatif Rashid Omar mwenye umri wa miaka minane kitendo ambacho ni kosa kisheria.
Mbali na makosa hayo, mshitakiwa huyo alidaiwa kumshambulia kwa kumbinya mkono wake wa kulia na kumchoma sindano Nurdin Seif Hamad mwenye umri wa miaka mitano na kumsababishia maumivu mwilini mwake.